FAMILIA ya Ndesamburo yakanusha kuwapo mgogoro wa rambirambi ya kati yao na CHADEMA


Familia ya mbunge wa zamani wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo imeushtukia mchezo mchafu unaochezwa kuhusu rambirambi za kifo cha mwanasiasa huyo na kuwajia juu wanaozusha kuwapo kwa mgogoro kati ya familia hiyo na Chadema.

Mtoto wa marehemu, Lucy Owenya alisema jana kuwa uzushi huo unalenga kuichonganisha familia hiyo na viongozi wa kitaifa wa Chadema akiwamo Mwenyekiti Freeman Mbowe.

Katika baadhi ya mitandao ya kijamii, kuna taarifa zinazodai kuibuka kwa sintofahamu kati ya familia ya marehemu na viongozi wa Chadema akiwamo Mbowe na Katibu Mkuu wake, Dk Vincent Mashinji.

Taarifa hizo ambazo zimekanushwa vikali na familia, zinadai kiasi cha rambirambi kilichochangwa ndani na nje ya nchi ni zaidi ya Sh600 milioni, lakini familia imekabidhiwa Sh120 milioni tu.

Kwa mujibu wa madai hayo, fedha za rambirambi zinazodaiwa kuchangwa bila kupitia mikononi mwa familia ni zaidi ya Sh600 milioni, huku ikidaiwa Sh345 milioni zikichangwa kutoka Ujerumani.

“Sisi kama wanafamilia tunajiweka mbali na ujumbe huo wa kizushi wa namna hiyo wenye malengo mabaya ya kuichonganisha familia na mwenyekiti wetu Freeman Mbowe,” alisema Owenya. “Ukitazama ni kama wanataka kuibua hoja fulani kuwa kwa vile upande fulani kule Arusha ulituhumiwa kula fedha za rambirambi basi na huku tuwazushie viongozi wa Chadema.”

Ingawa hakufafanua, lakini rambirambi zilizoibua manung’uniko ni za wanafunzi na walimu wa Lucky Vincent ya Jijini Arusha, ambao walipoteza maisha na zaidi ya Sh300 milioni zilichangwa.

Ndesamburo ambaye alikuwa Mbunge wa Moshi Mjini kwa vipindi vitatu mfululizo (2000-2015), alifariki dunia Mei 31, alipofikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.

Mwanasiasa huyo, alikuwa ofisini kwake Hoteli ya Keys, Moshi akitaka kusaini hati ya malipo, kwa ajili ya kukabidhi rambirambi kwa vifo vya wanafunzi wa Lucky Vincent.

Ilikuwa akabidhi Sh100,000 kwa kila familia iliyopatwa na msiba huo na ilikuwa akabidhi fedha hizo kwa Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro ambaye alikuwa naye ofisini hapo. “Hata arobaini haijaisha wanaanza kuturudishia uchungu wa kumpoteza mzee kwa kueneza mambo ya uongo. Wamwache mzee (Ndesamburo) apumzike kwa amani. Wasitafute kick (sifa),” alisema Owenya.

Owenya ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), alikataa kutaja kiasi cha rambirambi kilichopatikana lakini akasisitiza kuwa wanaangalia njia bora za kisheria za kushughulikia suala hilo.

Akizungumzia suala hilo, Katibu wa Chadema Mkoa Kilimanjaro, Basil Lema alisema katika dhambi mbaya ambayo waliosambaza ujumbe huo wameipata, ni kuichonganisha Chadema na familia ya marehemu mzee Ndesamburo.

Lema, ambaye alikuwa Katibu wa Ndesamburo katika kipindi chote ambacho mzee huyo alikuwa mbunge, alisema taarifa za kutafunwa kwa rambirambi ni uongo na kulaani waliousambaza ujumbe huo.

Katibu huyo alisema Chadema makao makuu ndiyo iliyobeba kwa sehemu kubwa gharama za msiba huo na kwamba kila kiongozi wa Chadema aliyefika msibani alijigharamia.

Chanzo: Mwananchi
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad