Serikali kupitia Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe imelifungia gazeti la Mawio kuchapishwa kwa miezi 24 kuanzia leo (Alhamisi).
Taarifa iliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dk Hassan Abbas imesema waziri amechukua hatua hiyo kwa mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa kifungu cha 59 cha Sheria ya Huduma za Habari namba 12 ya mwaka 2016.
Amesema hatua hiyo inatokana na gazeti hilo katika toleo namba 196 la 15-21 Juni, 2017 kuchapisha katika ukurasa wa mbele picha za marais wastaafu Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete ikiwahusisha na sakata la mchanga wa madini.
Pia, katika ukurasa wa 12 wa gazeti hilo limechapisha makala iliyoandikwa Lissu: Mkapa, Kikwete wataponaje? Kuwatuhumu viongozi hao kuhusika katika sakata la madini wakati ukweli ni kwamba hawakuwa sehemu ya uchunguzi wa kamati za Rais John Magufuli na wala matokeo ya kamati hizo hayakuwatuhumu kwa kosa lolote.
Taarifa ya Waziri Mwakyembe kwa mhariri mkuu wa gazeti hilo imesisitiza kuwa, licha ya utetezi wao, habari hizo si tu zimekiuka agizo la Serikali lakini pia, zimekiuka vifungu vya 50(a), (b), (c), (d) na (e) vinavyokataza uandishi wenye dhamira hasi.
“Sina budi kulifungia gazeti lako na kukutaka usitishe kulichapisha kwa nakala ngumu au ya mtandaoni kwa kipindi cha muda wa miezi ishirini na nne 24 tangu tarehe ya barua hii kwa mamlaka niliyopewa chini ya sheria ya huduma za habari namba 12 ya mwaka 2016 kifungu 59,” imesema taarifa ya Dk Mwakyembe kwenda kwa mhariri wa Mawio.
Waziri pia amevipongeza vyombo vingi vya habari ambavyo amesema kuanzia leo vimefuata weledi wa taaluma na misingi ya sheria, vikitii agizo la Serikali kwa kutowaingiza katika sakata hilo pasipo hoja za msingi viongozi wastaafu.