Gor Mahia ya Kenya imefanikiwa kuwa timu ya kwanza kutwaa ubingwa wa SportPesa Super Cup baada ya kuifunga AFC Leopards kwa mabao 3-0 kwenye mchezo wa fainali uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam leo Jumapili.
Mchezo huo ulizikutanisha Gor na Leopards ambao ni watani wa jadi nchini Kenya maarufu kama Mashemeji. Ushindi huo uliwafanya Gor kupachikwa jina la ‘mashemeji wa kweli’.
Mabingwa hao waliondoka na kiasi cha Sh60 milioni kama zawadi pia kupata fursa ya kucheza na Everton ya England kwenye mchezo wa kirafiki utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Julai 13.
Kipigo kwa Leopards kiliongeza uchungu kwani kimewafanya kufungwa idadi kama hiyo ya mabao mara mbili mfululizo katika kipindi cha wiki tano, jambo ambalo limewaweka katika wakati mgumu.
Katika michuano hiyo, timu za Simba na Yanga ziliaga mapema baada ya kufungwa na timu za Nakuru All Stars na AFC Leopards hivyo kutoa fursa kwa Mashemeji hao kukutana.