Baada ya mbio ndefu za michuano ya SportPesa Super Cup hatimaye Jumapili hii Klabu ya Gor Mahia kutoka nchini Kenya wamechukua kombe hilo kwa ushindi wa goli 3-0 dhidi ya mahasimu wao, AFC Leopards ambao pia wanatoka nchini Kenya.
Gor Mahia wamepata goli lao kwanza kupitia kwa mshambuliaji wao Otieno Philemoni kunako dakika ya 18 kipindi cha pili. Timu hiyo iliongeza kasi zaidi na kujipatia magoli mengine wawili na kuufanya mchezo huo kumalizika kwa kuwafunga AFC Leopards goli 3 kwa nunge.
Gor Mahia kwenye safari yake mpaka kufika fainali ya SportPesa Super Cup imezitoa klabu za Jang’ombe Boys kutoka Zanzibar na Nakuru All Stars .
Kwa ushindi huo klabu ya Gor Mahia imeibuka na kitita cha Dola elfu 30,000 za kimarekani na imepata nafasi ya kuchuana na Klabu ya Everton kutoka England Tarehe 13 July mwaka huu.
Michuano ya SportPesa Super Cup imeandaliwa na Kampuni ya kubashiri ya SportPesa ambao ni wadhamini wa Klabu za Simba SC, Yanga SC pamoja na Singida United zote kutoka Tanzania na jumla ya timu 8 zilishiriki michuano hiyo ambapo timu zote nne kutoka Tanzania zilitolewa.