ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Glory of Christ Tanzania Church (GCTC) ‘Ufufuo na Uzima’, Askofu Josephat Gwajima, amejitapa hadharani kuwemo kwenye kumi bora ya orodha ya matajiri wakubwa wenye viwango vya umilionea nchini, kauli iliyopokelewa kwa hisia tofauti miongoni mwa waumini na watu mbalimbali, Amani linawasilisha.
Jumapili ya wiki iliyopita, mwandishi wetu alihudhuria ibada ya askofu huyo ambaye alianza kwa mbwembwe na majigambo makubwa ya ‘kumvua‘ mtu taulo, jambo ambalo hakulifanya kwa madai ya kuelekeza nguvu kwenye ishu ya mchanga wa dhahabu, ambapo pamoja na mambo mengine, Gwajima alimshukuru Mungu kwa ukwasi wa kutisha alionao na kuwataka Watanzania kuamka na kuzitumia fursa za kimaendeleo zilizopo nchini.
Akitembea kwa madaha na kuhubiri kwa mikogo na staili mbalimbali za madoido kama ilivyo ada yake, mchunga kondoo huyo wa Bwana mwenye ‘madini’ ya kutosha kichwani, alisema tatizo kubwa la Watanzania ni kutegemea miujiza ya mafanikio kuliko kujitolea kufanya kazi ndiyo maana wengi hubaki maskini licha ya kuwa na kila sifa ya mafanikio ikiwemo usomi wa kiwango cha juu.
“Namshukuru sana Mungu kwamba miongoni mwa mamilionea 10 nchini Tanzania na mimi nimo, hilo halina shaka kabisa yaani nasema kwa msisitizo nimo kwenye orodha ya matajiri 10 wa nchi hii. Unajua ngoja niweke wazi jambo moja muhimu, nchi yetu imejaaliwa kuwa na rasilimali nyingi sana, tatizo letu ni mafundi wa kuongea na si kufanya kazi, tunategemea miujiza kutoka kwa Mungu.
“Mungu mwenyewe alisema nitabariki kazi za mikono yenu, hakusema nitawabariki kwa kukaa bila kufanya kazi, mimi namshukuru kwa alichonijaalia maana nafurahia maisha na wewe unayenisikiliza nakuomba uamke upambane na maisha, maana Tanzania ina kila kitu, mito na maziwa kwa kilimo, ukichimba shimo hadi kiunoni, kwa wale wakazi wa Shinyanga unapata madini, tuamke na tufanye kazi ndipo tuwe na pesa, mimi ninao utajiri wa kutosha,” alisema Askofu Gwajima. Miongoni mwa matajiri wakubwa wanaotajwa kuongoza nchini Tanzania, ni pamoja na Mohamed Dewji, ambaye ni Mkurugenzi wa Mohamed Enterprises Tanzania Limited (MeTL), Rostam Aziz, mfanyabiashara wa masuala ya madini na Dk. Reginald Mengi, mwenyekiti wa Makampuni ya Industrial Products Promotions (IPP). Wengine ni Said Salim Bakhressa, Mwenyekiti wa Azam Group of Companies, Yusuf Manji ambaye ni Mwenyekiti mstaafu wa Quality Group na wengine wengi.