HATIMAYE mwili wa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Salum Almas (28), unatarajiwa kuzikwa leo ikiwa ni siku takribani ya 50 tangu kuuawa na polisi kwa tuhuma za ujambazi.
Almasi ambaye alikuwa mwanafunzi wa chuo hicho Kituo cha Kompyuta (UCC), akichukua masomo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (IT), aliuawa na polisi jirani na mashine ya kutolea fedha ya kielektroniki (ATM) ya benki ya CRDB iliyopo kandoni mwa ofisi za Uhamiaji, Kurasini kwa madai ya kutaka kupora fedha.
Mwili wake ulihifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Mjomba wa marehemu, Tulleyha Abdulrahman, aliiambia Nipashe jijini Dar es Salaam jana kuwa mwili huo ulikuwa ukifanyiwa uchunguzi Muhimbili jana, chini ya mwanasheria wa familia, ndugu, polisi, tume ya haki za binadamu na kiongozi kutoka Serikali ya Mtaa wa Kurasini ambako ndiko marehemu alikuwa akiishi.
Awali, baada ya mauaji ya Salum, ndugu waligoma kuuzika mwili huo wakitaka Jeshi la Polisi limsafishe mtoto wao dhidi ya tuhuma za ujambazi kwa maelezo kuwa kijana huyo hakuwahi kujihusisha na vitendo hivyo katika maisha yake.
Hata hivyo, baada ya kuuawa kwa Almasi, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salam, Simon Sirro (sasa ndiye Mkuu wa Jeshi hilo, IGP), aliwataka wale wanaobisha kuwa kijana huyo hakuwa jambazi waende eneo la tukio kuwauliza mashuhuda.
Licha ya kauli hiyo, ndugu wa marehemu waligoma kuuchukua mwili huo na hatimaye walimwandikia barua Rais John Magufuli pamoja na Mkurugenzi wa Upelelezi Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, wakisisitiza kuwa Almasi aliuawa kimakosa kwa sababu hakuwahi kuwa jambazi na hivyo, wakataka Polisi wamsafishe ndipo wamzike.
Wiki mbili zilizopita, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Boaz alithibitisha makao makuu kufanya uchunguzi dhidi ya tukio hilo.
“Ni kweli tunachunguza ili kuthibitisha ukweli ni upi. Ndugu walituandikia barua ya malalamiko ya kuuawa ndugu yao wakati siyo jambazi. Bado uchunguzi unaendelea…haujafikia mwisho, tukimaliza watataarifiwa. Ila kila mara tumekuwa tukiwapa mrejesho,” alisema DCI Boaz.
Mjomba wa marehemu, Abdulrahman, alisema jana kuwa baada ya uchunguzi huo, wanatarajia kumzika mtoto wao Ijumaa (kesho) katika makaburi ya Kisutu.
“Leo (jana) tupo hapa Muhimbili. Mwili wa Salum unafanyiwa uchunguzi kabla ya kuzikwa. Hivyo ndivyo naweza kukueleza kwa sasa… ila tutazika Ijumaa makaburi ya Kisutu,” alisema.
Abdulrahman ambaye ndiye aliyekuwa akiishi na Salum enzi za uhai wake eneo la Kurasini, Shimo la Udongo, wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, alisema baada ya uchunguzi huo watazika wakati wakingojea majibu ya uchunguzi.
Awali, akisimulia kuhusu tukio hilo, Abdulrahman alisema Salum aliuawa muda mfupi baada ya (yeye) kumpigia simu amfuate kituo cha daladala cha JKT kwa ajili ya kuchukua fedha za matumizi za nyumbani.
“Tulionana saa 3:30 asubuhi Jumapili baada ya kumtaka aje kituo cha daladala cha JKT, nilimpatia Sh. 30,000 akaondoka kurudi nyumbani, saa nane baadaye nikapigiwa simu kujulishwa kuhusu kifo chake,” alisema siku hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi iliyotolewa siku moja baada ya mauaji hayo ilieleza kuwa kijana huyo aliuawa wakati akijaribu kupora fedha za benki ya CRDB zilizokuwa zinasambazwa na gari la kampuni ya G4S katika mashine zake za kutolea fedha, huku majambazi watatu waliokuwa katika pikipiki mbili wakikimbilia kusikojulikana.