Hatimaye Kilichomuua Ndesambuo Chaanikwa..Mbowe Aeleza A - Z ya Saa Mbili Kabla ya Kifo Chake Alivyokuwa..!!!


HATIMAYE taarifa za uchunguzi wa awali kuhusiana na kile kilichosababisha kifo cha ghafla kwa mbunge wa zamani wa Moshi Mjini na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Kilimanjaro, Philemon Ndesamburo, zimetolewa na kuonyesha kwamba alipata tatizo la moyo.

Ndesamburo alifariki dunia katika Hospitali ya Rufani ya KCMC mkoani Kilimanjaro jana alikopelekwa baada ya kuzidiwa ghafla akiwa ofisini kwake, katika jengo la hoteli yake ya Keys iliyoko mjini hapa.

Kiongozi wa jopo la madaktari walioufanyia uchunguzi mwili wa kiongozi huyo, Prof. Elisante Massenga, alisema jana kuwa taarifa ya awali ya uchunguzi inaonyesha kuwa kifo cha ghafla cha Ndesamburo kimetokana na matatizo ya moyo.

bila kufafanua zaidi, Prof. Massenga alisema bado walikuwa wakieendelea na uchunguzi uliokuwa ukihusisha vipimo mbalimbali na kwamba baada ya hapo ndipo watakapotoa taarifa kamili kwa wahusika.

MBOWE ASIMULIA KILICHOTOKEA
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema Ndesamburo, ambaye pia alikuwa mmoja wa wafanyabiashara wakubwa mkoani Kilimanjaro, alifariki dunia baada ya kuanguka ghafla wakati akitaka kuandika hundi ya fedha ya Sh. milioni 3.5 ikiwa sehemu ya mchango wake kwa Meya wa Arusha, Kalist Lazaro, ili akazikabidhi familia za watu wote waliopoteza ndugu zao katika ajali ya basi la shule ya Lucky Vincent ya Arusha iliyoua watu 35; ambao ni wanafunzi 32, walimu wawili na dereva wao.

Akisimulia zaidi, Mbowe alisema alifariki dunia jana saa 4:45 asubuhi baada ya kufikishwa KCMC.

“Mzee Ndesamburo alikuwa Dodoma kwenye vikao vya Baraza Kuu na alirejea juzi (Jumatatu) Moshi na jana (juzi) jioni akiwa mzima wa afya kabisa, alimpigia simu Meya wa Arusha, Kalist Lazaro, akimhitaji wakutane leo (jana) asubuhi saa tatu ofisini kwake Moshi ili aweze kumpatia mchango wa rambirambi ya marehemu waliopata ajali ya Lucky Vincent kule Arusha,” alisema.

Mbowe aliongeza kuwa baada ya hapo, Meya Lazaro alikwenda kumuona marehemu Ndesamburo jana majira ya saa nne asubuhi ofisini kwake katika Hoteli ya Keys.

“Wakaanza mazungumzo ofisini kwake ambayo yalikuwa ya kawaida na hatimaye akamuuliza wale victim (waathirika) wa Lucky Vincent wako wangapi?'… akamwambia wapo 35 (waliokufa) na akamwambia atampa mchango wa Sh. 100,000 kwa kila mfiwa,” alisema

Mbowe, akitaja kiwango cha jumla cha rambirambi hiyo kuwa ni Sh. milioni 3.5.

“Wakati Mzee anachukua kalamu kuandika hundi, kalamu ikamdondoka… akaanza kupoteza nguvu na Meya akanyanyuka kumshika na kumuuliza 'Mzee upo salama?' Akamjibu 'nipo salama',” alisema Mbowe.

Alieleza zaidi Mbowe kuwa hata hivyo, Mzee Ndesamburo aliendelea kulegea na kuishiwa nguvu, hali iliyomlazimu Meya kuwaita wafanyakazi wa hoteli hiyo na ambayo ni yake na familia, kwa ajili ya kumpa huduma ya kwanza.

“Walimkimbizia Hospitali ya Rufani ya KCMC na alipofika, walimpokea na kumwekea kifaa cha kupumulia ili kuokoa maisha yake. Lakini baada ya nusu saa, madaktari walisema Mzee amefariki… hawakuweza kuokoa maisha yake,” alisema.

Mbowe alisema chama hicho kimepoteza mmoja wa waasisi wao, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro na mjumbe wa Baraza Kuu la chama.

“Pia alikuwa Mbunge wa Moshi tangu mwaka 2000 hadi 2015. Sisi kama Chadema tumepokea kwa mshtuko mkubwa sana kuondoka kwa mzee Ndesamburo hasa ukizingatia amekuwa ngome ya chama kwa muda mrefu, mshauri na msaada wa chama kwa muda mrefu,” alisema.

Kiongozi huyo wa Chadema alisema bado wanafanya mawasiliano na viongozi wa chama na familia namna ya kushiriki ipasavyo katika msiba huo kwa kuwa Mzee Ndesamburo anastahili kupewa heshima kwa kazi ambayo ameifanyia nchi na chama chake.

Awali, Katibu wa Chadema mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema, aliithibitishia pia Nipashe juu ya kifo cha Ndesamburo na kutoa maelezo yanayofanana na ya Mbowe, akifafanua kuwa eneo lilipo hoteli aliyofia Ndesamburo ni la Rau, Moshi Mjini.

Lema alisema kwao, kama chama mkoani Kilimanjaro, ni pigo kubwa la kisiasa hasa kwa siasa za Moshi Mjini na Kanda ya Kaskazini kwa ujumla wake na pia kwa taifa kwa sababu alikuwa mstari wa mbele katika kufanikisha harakati za mageuzi nchini.

Jana, wakati mwili wa Ndesamburo ukiendelea kufanyiwa uchunguzi na kuhifadhiwa kabla ya taratibu nyingine za kifamilia na mazishi, watoto wake wa kiume Sindato Philemon na Thomas ndio waliokuwa mstari wa mbele kuratibu shughuli zote hospitalini.

ALIKOANZIA
Akizungumzia historia ya Ndesamburo, ambaye alizaliwa Februari 19, 1935 kwenye siasa wakati wa uhai wake, Katibu wa Chadema mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema, alisema Ndesamburo alianza harakati za mageuzi mwaka 1988 wakati wa kudai mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977.

Lema alisema Ndesamburo aliipenda siasa tangu alipoamua kuacha kazi serikalini mwaka 1972, baada ya kupangiwa kazi ambayo hakuisomea ingawa alikuwa na shahada ya kwanza ya Uchumi wa Biashara katika Kilimo aliyoisomea London, Uingereza.

Baada ya mfumo wa vyama vingi kuanza mwaka 1992 Ndesamburo alikuwa miongoni mwa waasisi wa chama na miongoni mwa watu 10 wa kwanza waliojitolea kudhamini uanzishwaji wake.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 1995, Ndesamburo alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Taifa, Mjumbe wa Baraza la Wadhamini wa Chadema Taifa na Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Kilimanjaro.

Harakati za mwisho za Ndesamburo, kabla ya uhai wake alikuwa akiwania nafasi ya kuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini inayounganisha mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Tanga na Manyara yenye majimbo 35 ya uchaguzi.

Alikuwa anakwaana katika vita hiyo na Daniel Porokwa ambaye aliwahi kuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Manyara, kabla ya kujiunga na Chadema mwaka 2015.

ATAKUMBUKWA
Yako mambo mengi ambayo yatamfanya Ndesamburo akumbukwe, lakini kubwa zaidi ni kujitoa kwake kwa ajili ya jamii.

Msemaji wa familia ya Ndesambauro ambaye ni mwanawe wa kiume, Sindato Philemon, alisema baba yake ambaye ameacha watoto 11 wakiwamo wakiume watatu na wakike wanane, ni kuwajali watu na kutoa misaada pale ilipohitajika.

Sindato alisema baadhi ya misaada na huduma za msamaria mwema ambazo baba yake aliwahi kuzitoa wakati wa uhai wake ni pamoja na helikopta ambayo ilikuwa ikitoa huduma ya usafiri kwenda kwa Babu wa Loliondo mara nne kwa siku.

“Mzee (Ndesamburo) nakumbuka alitoa magari mawili ya kusafirisha wagonjwa bure pamoja na helikopta ambayo ilikuwa ikipeleka wagonjwa mara nne kwa siku kule Loliondo,” alisema Sindato.

Credit - Nipashe
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad