Hivi Ndivyo Rais Magufuli Alivyotengua Kauli ya Waziri Wake Ummy Mwalimu....

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli amesema kuwa chini ya utawala wake, haitotokea mwanafunzi aliyepata mimba akaruhusiwa kurudi shuleni kuendelea na masomo baada ya kujifungua.

Rais Magufuli amesema kuwa kwa kufanya hivyo itapelekea wanafunzi wengi kupata mimba wakiwa bado wapo shuleni kwa sababu wanajua wataruhusiwa kuendelea na masomo kitu ambacho yeye hawezi kukivumilia.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo alipokuwa akifungua barabara ya Bagamoyo – Msata yenye urefu wa kilomita 64 ambayo itasaidia kupunguza msongamano wa magari katika barabara ya Morogoro kwani ndiyo pekee iliyokuwa ikitumika kuingia na kutoka jijini Dar es Salaam.

Kwa kauli hiyo ya Rais Magufuli, ni dhahiri kuwa ametengua kauli iliyokuwa imetolewa na Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu Aprili 27 mwaka huu ambapo alisema kuwa, mwanafunzi hawezi kunyimwa haki yake ya elimu kwa vile tu amepata mimba akiwa shule.

Waziri Ummy Mwalimu alisisitiza kuwa wanafunzi wa kike wanaopata mimba wakiwa mashuleni waendelee na masomo yao ili kufikia malengo walioyanayo nchini.

Aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa maswala ya kijinsia ulioandiliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kitivo cha Ualimu (DUCE) alipomuwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

“Tunapokataza watoto wa kike wasiendelee na masomo pindi wanapopata ujauzito wakiwa mashuleni tunawaadhibu watoto wa masikini washindwe kutimiza malengo yao kwa wakati waliotarajia,” alisema Waziri Ummy.

Aidha, Rais Dkt Magufuli amezita Asasi za Kiraia (NGOs) zinazotaka wanafunzi wenye watoto waendelee na masomo, zijenge shule zao za kuwapeleka hao watoto lakini serikali yake haiwezi kutoa fedha kwa ajili ya elimu bure halafu mwanafunzi apate mimba bado serikali hiyo hiyo ichukue jukumu la kumsomesha mzazi.

Katika kutoa mbadala wa hilo, Rais Magufuli amesema wanafunzi hao wanaweza kujiunga na vyuo vya ufundi pindi wanapopata ujauzito ambapo vyuo hivyo vitawakubali lakini sio kuendelea na masomo tena.

Akizungumzia upande wa wanaowapa wanafunzi mimba, Rais Magufuli alisema kuwa sheria ipo wazi kwamba ni miaka 30.

Kauli hii ya kiongozi wa nchi imepokelewa kwa mtanzamo tofauti ndani na nje ya nchi, ambapo baadhi wamemuunga mkono kuwa wanafunzi wakijifungua wasirudi shule huku wengine, hasa wale watetezi wa haki za wanawake wakipinga kauli hiyo na kusema, huko ni kuwabagua baadhi ya watu kupata haki yao ya msingi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad