Kwa bajeti ya Sh31.7 trilioni, ongezeko la Sh40 katika mafuta lisingetegemewa kuibua mjadala mzito, lakini hali imekuwa tofauti; wako waliolipokea kwa mikono miwili na wako wanaolipinga kwa nguvu zote.
Ongezeko hilo lilitajwa wakati Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alipokuwa akieleza mapendekezo kadhaa ya sheria ya kodi na ushuru, na hasa kuondolewa kwa kodi ya leseni ya magari.
Ushuru huo sasa utalipiwa mara moja tu wakati wa kusajili gari.
Dk Mpango alisema badala ya kodi hiyo iliyoondolewa, ambayo ilikuwa kati ya Sh150,000 na Sh250,000, Serikali sasa itatoza Sh40 kwa kila lita ya mafuta ya taa, petroli na dizeli.
Awali ilionekana kama tozo hiyo itakuwa ya kuwasaidia wamiliki wa magari tu, lakini mjadala ulioibuka umetoa picha tofauti.
“Ushuru huo wa mafuta utapandisha bei za bidhaa na huduma na hivyo watakaoathirika ni wananchi wote,” alisema Profesa Honest Ngowi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe.
“Ushuru ulioongezwa katika mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa, utabebwa na kila mwananchi anayetumia bidhaa na huduma mbalimbali.”
Alisema ushuru huo utasababisha bei ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kupanda na kwamba gharama hiyo itafidiwa na mlaji wa mwisho ambaye ni mwananchi.
Alisema mmiliki wa gari ndogo ya abiria akipandishiwa gharama ya petroli kutokana na kuongezwa kwa ushuru huo, naye atapandisha bei ya huduma yake.
Alisema mwenye lori pia atapandisha gharama za kusafirisha bidhaa na mazao, hivyo gharama hizo zitafidiwa na mnunuzi wa mazao na bidhaa.
Alisema matokeo yake gharama za vyakula na bidhaa zinaweza kupanda ili kufidia ongezeko hilo la bei ya mafuta.
“Mafuta ni kila kitu, ukipanda daladala ukienda sokoni kununua vyakula, ukiwa mkulima au mfugaji utachangia gharama za ushuru wa mafuta,” alisema.
Dhana kama hiyo alikuwa nayo mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Haji Semboja, ambaye hata hivyo alisema mabadiliko hayo yatamuhusisha kila mtu katika kuchangia barabara badala ya wamiliki wa magari pekee.
“Kabla ya bajeti hii, kodi ya barabara ililipiwa na wenye magari, lakini sasa wapandaji wote wa magari watasaidiana na wamiliki kulipia gharama ya ushuru wa mafuta,” alisema.
Alisema utaratibu huo wa kushirikisha jamii yote kulipia kodi ni ubunifu mzuri wa kuipatia Serikali fedha nyingi zaidi kuliko ilivyokuwa ikifanyika awali kwa kuwabana wenye magari pekee yao.
Kwa upande wake, Godfey Mramba ambaye ni mtaalam wa kodi alisema ingawa ongezeko hilo si kubwa, kila mtumiaji wa barabara atachangia ushuru huo wa mafuta.
“Hii ina mwenye basi, mwenye bajaji na abiria watalipia gharama, mwenye trekta, mkulima na mlaji wa vyakula watalipia kupitia ushuru huu wa mafuta,” alisema.
Msomi mwingine aliyekubaliana na mabadiliko hayo ya kuondolewa kwa kodi ya magari ni Ali Mufuruki, ofisa mtendaji mkuu wa kampuni ya Infotech ya jijini Dar es Salaam.
“Sasa utalipia kodi kwa kadri utakavyotumia gari,” alisema Mufuruki katika mahojiano na gazeti la Mwananchi.
Alisema mtu asiyetumia gari maana yake hatanunua mafuta na hivyo hatalipia ushuru huo wa Sh40 kwa lita kwa kuwa hatatumia mafuta.
Mwenye mawazo tofauti alikuwa mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku, maarufu kwa jina la Msukuma, ambaye alishangazwa na kitendo cha Serikali kuitikia mapema kilio cha kuondoa kodi ya leseni za magari.
Akizungumza na kituo cha redio cha Clouds FM, Msukuma alisema suala hilo liliibuka katika kipindi cha maswali na majibu bungeni, lakini likakuzwa na mjadala.
Alisema anashangaa jinsi lilivyokuwa kubwa hadi Serikali ikakubali kuliondoa wakati wakulima wana malalamiko ya muda mrefu ambayo hayafanyiwi kazi.
Alisema kuondoa kwa kodi hiyo hakuwezi kuwanufaisha wakulima na wafugaji ambao sasa wanalazimika kupunguza ng’ombe kutokana na hali ngumu wakati kimila wanatakiwa watoe mahari hadi ya ng’ombe 100.
Wamiliki wa magari wanena
Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, mtu anayenunua gari lenye injini ya ukubwa wa cc 3,000, atalipia hadi Sh300,000 wakati akisajili badala ya Sh 250,000 ambazo angekuwa akilipia kila mwaka kwa mujibu wa sheria ya sasa.
Hali kadhalika kwa mtu atakayenunua gari lenye injini ya ukubwa wa cc 1501-2500 atakayelipia Sh250,000 badala wakati wa kulisajili na anayenunua gari la cc 501-1500 atalipia Sh200,000 badala ya Sh150,000 alizotakiwa kulipia kila mwaka.
Akizungumzia mapendekezo hayo, mmiliki wa gari aina ya Toyota Brevis yenye cc 3000, Nelson Mashambu alipongeza hatua hiyo kwa vile itawabana wajanja wachache waliokuwa wakitoa taarifa za uongo kwa Mamlaka ya Mapato nchini(TRA).
Mkazi huyo wa eneo la Kimara anayetumia kati ya lita 10-15 za mafuta kwa siku, alisema baadhi ya wamiliki wa magari wamekuwa wakitoa taarifa za uongo kwa TRA kwa kutoa idadi ndogo ya magari ili wakwepe kulipa kodi ya barabara.
“Mimi naona uamuzi huu ni mzuri kwa vile unaweza kumkuta mtu anamiliki magari matano lakini baadaye anaandika barua TRA akisema gari yake moja mbovu haitumii lakini sasa hata kama utadanganya utakamatwa kwenye mafuta,” alisema.
Hoja inayofanana na hiyo ilitolewa pia na mfanyabiashara anayejishughulisha na usafirishaji abiria , Richard Matiku.
Matiku, anayemiliki gari aina ya Toyota Hiace, alisema uamuzi huo umewaondolea usumbufu wananchi ambao wakati mwingine walilazimika kulipia kodi hata magari ambayo yalikuwa hayatembei.
Lakini alionyesha wasiwasi wake namna Serikali itakavyoweza kukusanya kodi hiyo inayokusudiwa kuongezwa kwenye mafuta akisema baadhi ya vituo vya kuuzia mafuta hayo havina mashine za kielektroniki.
Mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Robin Fungameza ambaye ni mkazi wa Kibaha alilalamikia mfumo huo mpya akisema unawabana wamiliki wengi wa magari.
“Hili jambo siliafiki hata kidogo. Fikiria mimi dereva natoka Dar narudi nyumbani Kibaha halafu njiani nakutana na bonge la foleni, itanilazimu kusimama ili nipate angalau bia chache kusubiria foleni,” alisema.
“Sasa unafika kwenye bia nako kodi imeongeza ...jamani sasa tutapumulia wapi?”
Si wazo baya hila kwangu mimi nahoji je sisi tuliolipia siku chache kabla la hawajatangaza kuitoa itakuwaje maana sina hata mwezi nimetoka kulipia 230,000/= je hapo inakuwaje??
ReplyDelete