JOHN Bocco alipokuwa Azam FC alikuwa akitumia jezi namba 19, lakini sasa ametua Simba ambapo jezi hiyo inatumiwa na kiungo mwenye uwezo mkubwa, Mzamiru Yassin, ambaye inadaiwa kuwa hataki kusikia akipokwa namba hiyo.
Mzamiru, ambaye amesajiliwa na Simba kutoka kwa Wakata Miwa wa Mtibwa Sugar, amekuwa akiitendea haki jezi hiyo yenye namba 19, kutokana na uwezo wake wa kusimama vema dimba la katikati, huku pia Bocco naye akifanya hivyo huko anakotoka.
Baada ya kusajiliwa Simba ndipo zikaanza kuzagaa taarifa kwamba huenda Straika huyo akakabidhiwa jezi aliyoizoea namba 19, lakini taarifa kutoka kwa watu wa karibu na Mzamiru zinadai kuwa, anaipenda jezi yake na hana mpango wa kuitoa kwa mtu mwingine.
“Sidhani kama Mzamiru atakubali kuachana na namba 19, kwani anaipenda sana, ngoja tuwaachie wenyewe, japo hakuna linaloshindikana kama wakikaa na kukubaliana,” alisema mchezaji mmoja wa Simba ambaye ni swahiba na Mzamiru.
DIMBA Jumatano lilikwenda mbali zaidi na kumtafuta Mzamiru, ambaye yupo kambini na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, nchini Misri, ambapo aliweka wazi kuwa hana mpango wa kuiachia jezi hiyo.
“Ni ngumu sana kulizungumza hili jambo, kama nitaendelea kubaki basi haitakuwa rahisi kuiacha, labda niwe nimeondoka katika kikosi cha timu hiyo,” alisema kiungo huyo.
Hata hivyo, taarifa nyingine kutoka Simba zinadai kuwa, wamemuandalia Straika huyo ambaye ameifanyia makubwa Azam FC, jezi namba 29 kama Mzamiru akikomaa na namba 19.
“Tumemuandalia jezi namba 29, kama ataipenda na kuridhika, kwani inawezekana Mzamiru akakataa kuachia namba 19, nadhani hakuna kitakachoharibika,” alisema kigogo mmoja wa Simba.
Credit - Dimba