Rais John Magufuli amewataka wakuu wa mikoa wote nchini kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa viwanda katika maeneo yao ili kuwawezesha wananchi kuongeza thamani ya mazao na kuzalisha ajira.
Rais ametoa agizo hilo leo (13 Juni, 2017) Ikulu jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na waakuu wa mikoa ya Tanzania Bara, kikao ambacho kimehudhuriwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Wengine waliohudhuria kikao hicho ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi na baadhi ya mawaziri.
“Mashamba yote yaliyotelekezwa, fuateni taratibu za sheria, yanyang’anyeni wapewe Watanzania ambao wapo tayari kuyaendeleza, lakini fanyeni jambo hili kwa kufuata utaratibu” amesema.
Pia, Magufuli amesema kila mkuu wa mkoa anapaswa kufanyia kazi fursa za uanzishaji wa viwanda katika eneo lake na kuhakikisha anashawishi wawekezaji kuzitumia fursa hizo kama inavyofanyika katika Mkoa wa Pwani ambako tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani viwanda vikubwa 83 vimejengwa na vingine kukamilika huku viwanda vidogo zaidi ya 120 pia vikiwa vimejengwa.
Pamoja na hilo, Rais Magufuli amewaagiza wakuu wa mikoa kuongeza juhudi za utatuzi wa migogoro ya ardhi ikiwa ni pamoja na kuharakisha mchakato wa kuwanyang’anya hati za umiliki wa mashamba makubwa ambayo yanashikiliwa na watu pasipo kuyaendeleza.
Amewatahadharisha wakuu wa mikoa hao dhidi ya watu wanaofanya njama za kujimilikisha maeneo makubwa ya ardhi na kusababisha wakulima na wafugaji kukosa maeneo ya kilimo na malisho na ametaka wote watakaobainika kufanya njama hizo wafichuliwe na kunyang’anywa maeneo hayo.
Kadhalika amewataka viongozi hao kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji na kuwahimiza wananchi kufanya kazi kwa juhudi na maarifa na kuzalisha chakula cha kutosha katika maeneo yao.
Katika kikao hicho wakuu wa mikoa wamempongeza Rais kwa juhudi zake za kuwapigania Watanzania hasa wanyonge na wamemuhakikishia kuwa wataendelea kumuunga mkono katika juhudi hizo ikiwemo kudhibiti wizi wa rasilimali za Taifa kama vile madini na maeneo ya hifadhi za wanyamapori.