KATAZO la Rais Magufuli, MSOMI Aeleza Jinsi Alivyopata Mimba Akiwa Shuleni na Alivyofanikiwa

Kama tamko la Rais John Magufuli lingetolewa mwaka 2002 wakati Caroline Kandusi akiwa kidato cha tatu, huenda leo asingekuwa na hadhi aliyo nayo sasa.
Asingewe kumalizia masomo yake baada ya kupata mimba akiwa na umri wa miaka 30 na hivyo angeweza kupoteza fursa nyingine zilizomuwezesha leo kuwa na shahada ya shahada ya umahiri katika uongozi akiwa na umri wa miaka 30.

Lakini walimu walimuwekea mazingira mazuri ya kujifungua na kurudi darasani kufanya mtihani, kitu ambacho kimekuwa ufunguo wa maisha na si ajabu kwamba sasa ni ofisa mipango wa taasisi ya kimataifa iliyo na ofisi zake nchini Canada.

Licha ya kupata ujauzito huo aliendelea na masomo na kufanikiwa kupata shahada ya kwanza na baadaye ya umahiri katika Uongozi na Utawala, kutoka Chuo Kikuu cha Jomo Kenyata kilichopo jijini Nairobi, Kenya.

Ingawa kwa muda mrefu watu wamekuwa wakijadili kuhusu watoto wa kike wanaopata mimba kurudi au kutokurudi shule, mjadala huo umepamba moto baada ya Rais Magufuli kusema: “Katika utawala wangu hakuna mwanafunzi atakayepata mimba, akarudi shule.”

“Baada ya kusikia tamko hilo nililia,” alisema Caroline alipoongea na Mwananchi kwa njia ya mtandao.“Rais asiwe na hofu ya wanafunzi wanaopata mimba kuambukiza wengine, hofu kubwa iwe kwenye nguvu kazi anayoipoteza.”
Alisema kwake, kupata nafasi ya kurudi shule kulimpa ari ya kusoma kwa bidii, kuwajibika na kumlea mtoto wake.“Kama ningechukuliwa kama mzinzi, nadhani nguvu kazi hii ingekuwa imepotea,” alisema.

Uhusiano na mwanafunzi mwenzake wakati wanaharakati wanajenga hoja kuwa mazingira huhuwalazimisha baadhi ya watoto wa kike kupata ujauzito wakiwa shuleni, Carloline anasema tatizo lake lilitokana na kuwa na uhusiano na mwanafunzi mwenzake (jina tunalihifadhi) wakati akiwa kidato cha tatu.

Anasema mwanafunzi huyo ndiye aliyempa mimba. Baada ya kubaini kuwa ana ujauzito, aliamua kukaa kimya kwa kuwa hakutaka ushauri wa yeyote kutokana na kuamini kuwa angepotoshwa zaidi. Aliendelea na masomo huku akiificha mimba kwa zaidi ya miezi saba bila kugundulika.


“Sikuwa na mabadiliko makubwa kiasi cha mtu kugundua. Sikuwa nikiumwa zaidi ya kutopenda kula,” anasema. Agosti 2002 mimba ikiwa na miezi saba, alikwenda kumuona daktari kwa mara ya kwanza na aliambiwa kuwa huenda akajifungua Oktoba 17. Hata hivyo, bado aliendelea kutunza siri. Walimu wamsaidia kwa kuwa hakuna marefu yasiyo na ncha, siku moja mwanafunzi mwenzake alimshika tumbo kwa bahati mbaya na kugundua kuwa Caroline ana ujauzito na alikwenda kuwataarifu walimu.

“Ghafla nikaitwa ofisi ya walimu wa kike, waliniweka kikao na kunihoji kuhusu ujauzito na bila kificho niliwaeleza ukweli,” alisema Caroline. “Wakati wanaigundua mimba, tayari ilikuwa na miezi tisa. Walimwita dada yangu anayeishi Dar es Salaam kwa kuwa wakati huo mama alikuwa safarini Ujerumani,” alisema.

Baada ya kugundulika, walimu wake walimpa ruhusa ya kwenda nyumbani ambako alishauriwa kuwekewa kidonge cha uchungu ili ajifungue mapema na kufanya mtihani wa kidato cha tatu. Lakini kabla ya kuwekewa, siku mbili baadaye yaani Oktoba 17 alijifungua.

“Walitaka kuniwekea kidonge cha uchungu, lakini siku za kujifungua zilikuwa zimefika na nilijifungua mtoto wa kiume tarehe 17 Oktoba kama daktari alivyoniambia,” alisema. Baada ya kujifungua alikwenda kuishi kwa dada yake jijini Dar es Salaam na alikuwa akitoka asubuhi kwenda shule na kurudi nyumbani. Kwa kuwa alikuwa katika mitihani ya mwisho wa mwaka ya kidato cha tatu, ilimbidi arudi shule wiki mbili baada ya kujifungua.

“Ilinibidi niwe nasoma daftari huku namnyonyesha mwanangu kwa sababu sikuwa na jinsi. Ilikuwa ni lazima nifanye mtihani na lazima nimlee mtoto wangu,” alisema Caroline. “Asubuhi nikiamka namnyonyesha mtoto, nakamua maziwa katika kichupa nayaacha kisha naenda shule.”

Uongozi wa Shule ya Cambridge ulimpa ushirikiano mkubwa Caroline na walimu hawakumpa kauli za kumkatisha tamaa, bali walimtia moyo na baada ya kujifungua, walikubali aendelee na masomo shuleni hapo hadi alipomaliza kidato cha nne.

Wazazi hawakumkaripiaBaada ya wazazi wake kufahamu kuwa Caroline ana ujauzito, walimhoji kutaka kujua mzazi mwenzake. “Niliwaambia wazazi wangu kuhusu jibu alilonipa huyo kijana na hawakuwa na la kufanya. Kwa kifupi hakukuwa na njia nyingine kwa sababu walifahamu kila kitu wakati tayari nimeshajifungua,” alisema.

“Kupata mimba si mwisho wa maisha. Bado binti mdogo anayepata mimba ana nafasi ya kuendelea na masomo na kufanikisha ndoto yake.” Caroline, ambaye alipata daraja la kwanza katika matokeo yake ya shahada ya kwanza, alisema wengi wanaopata mimba shuleni wanapoteza kila kitu kwa sababu wanakosa ushirikiano kuanzia shule, nyumbani na hata katika jamii na kukatishwa tamaa.

“Kauli nyingi wanazopata wasichana ni za kukatisha tamaa, jambo ambalo linawafanya wasichana wengi waendelee kufanya ngono kwa siri na kuendelea kutoa mimba,” alisema. Alisema mara nyingi jamii huwahukumu wasichana waliopata ujauzito wakiwa wadogo na kuwaona kuwa ni wakosefu, wazinzi na wahuni jambo linalowafanya wakate tamaa na kupoteza vipaji vyao.

Ageukia mafunzo kwa wasichana baada ya kupitia hayo yote, Caroline anaona hana budi kutumia muda wake wa ziada kuwafundisha wasichana wadogo shuleni jinsi ya kujitambua na kuepukana na changamoto za balehe.

“Bila hivyo mimba za utotoni zitaendelea kuongezeka na tutapoteza wasichana wengi ambao wangeweza kuwa viongozi au wanataaluma bora,” anasema.
Kwa sasa, Caroline anamsomesha mtoto wake anayeitwa Emmanuel mwenye umri wa miaka 14.

“Kumlea peke yangu ni changamoto kubwa hasa wakati anapomuulizia baba yake, lakini najitahidi kila niwezavyo,” anasema. Caroline, ambaye kwa sasa ameolewa na kupata mtoto mwingine, anatoa mfano wa jinsi jamii ilivyo na mtazamo hasi kuhusu wasichana waliozaa katika umri mdogo.

“Ukiwaambia watu kuwa una miaka 30 halafu una mtoto wa miaka 11 wanakuambia heee ulianza mapema?” alisema. Hata hivyo, anasema hakuwahi kuficha kuwa ana mtoto alipokuwa sekondari na alipoingia chuo kikuu, bali alimchukulia mtoto wake kama changamoto iliyompa ari ya kusoma kwa bidii.

Ushuhuda wa mama Rebecca Kandusi, ambaye ni mama wa Caroline, anasema hakuweza kumkasirikia au kumtelekeza binti yake baada ya kupata ujauzito kwa kuwa kila binadamu hufanya kosa. “Najua ni shetani aliyempitia. Kwa kosa lake, sikuweza kusema namsusa au namfokea, hapana. Niliendelea kumsupport kwa kila hali na kuendelea kumlea vyema,” anasema.


“Nimemlea katika misingi ya kidini ya kumjua Mungu na ninaamini kazi ya shetani ilikuwa ni kuona anaharibikiwa, lakini haikuwa hivyo.” Mama huyo anasema wazazi wanapowasusa au kuwakasirikia watoto baada ya kupata ujauzito, wanawaharibia mustakabali wa maisha yao.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad