Dodoma. Kauli ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kuhusu mgawanyo wa bajeti katika majimbo yanayoongozwa na wapinzani imezidi ‘kulipasua’ Bunge baada ya pande mbili za kisiasa kushambuliana ndani ya chombo hicho jana.
Jumanne wiki hii, muda mfupi kabla ya kupitishwa kwa Bajeti Kuu ya Serikali, Spika Ndugai alisema kupiga kura ya hapana katika bajeti hiyo ni kukataa fedha za maendeleo.
Wakichangia Muswada wa Sheria ya Fedha ya 2017 jana, pande mbili za wabunge, wa CCM na upinzani waliendelea kulumbana kuhusu suala hilo.
Mbunge wa Babati Mjini (Chadema), Pauline Gekul ndiye aliyelianzisha kwa kusema kuwa Bunge linaongozwa na kanuni na kwamba kupiga kura jambo lolote ni hiari.
“Nyie Serikali mnaongoza na sisi ni wapinzani tunaotegemea kuingia madarakani, hatuwezi kuunga mkono bajeti yenu, hili ni wazi. Hata keshokutwa mkawa upinzani mnaweza kuwa na mawazo yenu mbadala na msiunge mkono ya kwetu,” alisema.
“Nilishangaa sana, haijawahi kutokea mwongozo mmoja mtu akiomba wanapewa wengine sita the same (sawa)... ndiyo maana ilitushangaza sana na bahati mbaya mlifanya zile siasa mkiwa mmeachia wazi televisheni.”
Alisema Watanzania waliona kuhusu ubaguzi uliofanywa wa kuwataka wanapopelekewa jambo katika vikao vyao vya chama, kujiongeza.
“Leo nchi nzima miji mikubwa tunaongoza sisi wapinzani mkiamua kwa kauli zenu za ubaguzi ndugu zetu mlioko madarakani na sisi tukaamua kukusanya kodi zetu wenyewe (katika halmashauri zinazoongozwa na upinzani) tutashindwa?”
Alisema wakiamua kukusanya kodi za majengo na mabango ambazo Serikali Kuu imekuwa ikichukua na kutorudisha katika halmashauri, wataweza kugharamia shughuli za maendeleo katika halmashauri wanazoongoza.
“Mnawaambia Watanzania kwamba mtakusanya (kodi) katika miji yetu hamtoturudishia na tukienda kwa Watanzania tukawaambia msilipe kodi je? Mlianza na waliwaona mlipowaambia wasipeleke maendeleo kwenye majimbo ya wapinzani.”
Alisema kauli hiyo inaleta matatizo katika Taifa na kwamba kwa kauli hiyo, wamejichonganisha na kujichora kwa Watanzania.
“Na hii ni aibu, tunafahamu mlishaanza siku nyingi. Posho ya mfuko wa jimbo huku wapinzani mmeshaanza kutukata mmejiongezea nyinyi. Nilishaliombea mwongozo hapa. Mlishaanza iko wazi,” alisema.
Alisema wapinzani wako tayari kukusanya fedha katika majimbo yanayoongozwa na wapinzani na kutorejeshwa.
“Msifanye siasa za kitoto, Watanzania wanawaona. Mnatia uchungu tatizo hili,” alisema Gekul.
Hata hivyo, akichangia muswada huo, Mbunge wa Mtwara Vijijini (CCM), Hawa Ghasia alisema hakuna ubaguzi katika Bunge hilo na kwamba walichouliza na kukisimamia ni suala la kukaa miezi mitatu wanajadili bajeti wakitoa mapendekezo na Serikali kukubali halafu mmoja wa wabunge anasema haungi mkono.
Alisema kulikuwa na njia tatu ikiwa ni pamoja na kusema hapana, ndio na sina uamuzi ambayo inamaanisha yapo mambo mtu anayakubali na mengine hakubaliani nayo.
“Lakini hakuna mtu ambaye alisema hana uamuzi na badala yake wanakataa,” alisema na kukatishwa na mbunge aliyekuwa akiomba taarifa hatua ambayo ilimkera na kusema, “Naomba mtulie, kama sindano imeingia simtulie.” Ghasia aliendelea, “Waswahili wanasema ukilikoroga lazima ulinywe, tumeikataa bajeti kwa hiyo madhara ya kuikataa bajeti lazima yawafikie.
“Nashukuru naona sindano zangu zimeingia vizuri sana na ndiyo maana watu wote wanashindwa, wanagumia kama vile watoto wakichomwa sindano wanalia, poleni sana mwakani mjifunze jinsi ya kuunga mkono bajeti.”
Hata hivyo, kabla ya kuahirisha kikao cha asubuhi, Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisema kanuni ziko wazi za namna ya uendeshaji wa Bunge. “Ikiwa kiti kimefanya uamuzi, au jambo ambalo huridhiki nalo kanuni ya tano inakupa utaratibu wa kufanya.
“Si jambo zuri kabisa mtu aliyekuwa amekaa kwenye kiti unatoa maelezo kuhusu mtu huyo akiwa si yeye aliyeketi katika kiti wakati kanuni zinaelekeza nini cha kufanya.”
Alifafanua kuwa aliyekalia kiti kwa wakati husika ndiye mwenye mamlaka na kama mbunge hakubaliani na jinsi alivyotumia mamlaka, kanuni ya tano inampa utaratibu wa kufuata.
“Hoja ya kuhusu ubaguzi kama kuna mtu ana hoja hiyo achukue kanuni ya tano aisome afuate utaratibu,” alisema.
“Hatuwezi kuendelea kuijadili hoja hiyo hapa ndani kana kwamba haikuamuliwa. Kwa hiyo tusiilete kwa namna ambayo tunaenda mbele tunarudi nyuma.”
Kuhusu hoja ya kwamba kiti kilitoa nafasi ya mwongozo kurudiwa na zaidi ya mbunge mmoja, Dk Tulia alisema pande zote mbili (CCM na upinzani) walisimama wabunge wengi na kuzungumzia jambo hilohilo moja.
“Si jambo la kulaumu upande mmoja, uzuri nilikuwapo na majina ya wabunge waliozungumza ninao ni mbunge mmoja tu na huyo nitamtaja kwa sababu alifanya jambo jema alisimama na kusema jambo limeshazungumzwa,” alisema.
Kwa mujibu wa kanuni ya tano, kipengele kidogo cha nne, mbunge ambaye hakuridhika na uamuzi wa Spika anaweza kuwasilisha sababu za kutoridhika kwa Katibu wa Bunge ambaye atawasilisha malalamiko yake kwa Spika.
Kipengele kidogo cha tano kinasema Spika atawajibika kuitisha kikao cha Kamati ya Kanuni za Bunge na kulijulisha Bunge kuhusu uamuzi utakaotolewa na kamati hiyo.
Lakini kipengele kidogo cha sita kinasema Spika au Naibu Spika hatakuwa mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni za Bunge inapokaa kujadili uamuzi unaolalamikiwa, bali wajumbe watachagua mwenyekiti wa muda kwa asilimia 50 ya kura za siri.