Uteuzi wa IGP Simon Sirro kushika wadhifa umewaibukia wakazi wa wilaya za Kibiti na Mkuranga ambao wameamua kutoa ya moyoni.
Wakazi hao ambao wamefurahishwa wameeleza kuwa iwapo mkakati wake ni kukomesha mauaji ya wananchi yanayoendelea katika maeneo hayo basi aanze na mazungumzo kabla ya hatua zingine.
Mkazi wa Kibiti aliyejitambulisha kwa jina la Alhaji Msumi alisema IGP Sirro anapaswa kufika katika wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga kisha kufanya mazungumzo na wazee katika vijiji vya Bungu, Kibiti na Ikwiriri.
Amesema iwapo atafanya hivyo atabaini ni nini sababu ya mauaji hayo na wahusika wanaoendesha mauaji hayo na suluhisho lake.
Mzee mwingine wa Ikwiriri ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema uzoefu wa Sirro katika utulizaji na utatuzi wa matatizo utafanikisha kuwabaini watu au kikundi wanaoendesha mauaji katika wilaya hizo.
“Tunafahamu uzoefu alionao IGP Sirro, hivyo tunaimani suala la mauaji atalikomesha mara moja,” alisema.
Alisema kwa muda mrefu polisi walikuwa wakijua wilaya hizo hazipo salama kutokana na kukumbwa na matukio ya mauaji mara kwa mara,lakini walikuwa wazito kuanza kuusaka mtandao huo hadi pale yalipotokea mauaji ya aliyekuwa Ofisa Upelelezi Wilaya ya Kibiti, Peter Kubezya na wengine wawili ndipo walipoanza kuchukua hatua huku wakiwa wamechelewa.
Wenyeviti wawili wa Serikali za mitaa kupitia CCM waliopo katika Kata ya Kibiti ambao hawakutaka majina yao kutajwa gazetini wakizungumzia uteuzi wa IGP Sirro na kauli aliyoitoa walisema wanampongeza kwa kuonyesha moyo wa kutaka kuwakamata watu wote wanaojihusisha na mauaji katika wilaya hizo.
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Gullamuhussein Kifu alisema hali ya usalama inazidi kuimarika siku baada ya siku na kuwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kuwakamata watuhumiwa wote.