KAIMU Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la Global Resource Alliance, Madaraka Nyerere, ameiomba serikali kupunguza kodi katika bidhaa zinazotengeneza nishati ya jua.
Alisema hatua hiyo itawawezesha wananchi vijijini kupata nishati hiyo na hivyo kupungu za matumizi ya kuni na mkaa inayochangia kuharibu misitu.
Alikuw akizungumza hivi karibuni katika wiki ya maadhimisho ya mazingira iliyofanyika kitaifa wilayani hapa.
Madaraka alisema shirika lake kwa kushirikiana na Kampuni ya GoSol Ltd kutoka Finland limebuni jiko la kutumia mionzi ya jua.
Alisema jiko hilo litakuwa ukombozi kwa wajasiriamali wadogo vijijini ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za umeme, mafuta na gesi.
Akifafanua faida ya jiko hilo linalotumia vioo vya kawaida kukusanya mionzi ya jua, Meneja Mradi wa GoSol kutoka Finland, Heikki Lindfors, alisema jiko hilo ni ukombozi kwa wakazi wa vijijini zaidi ya bilioni tatu duniani.
Alisema jiko hilo linaweza kuokoa zaidi ya tani tisa ya miti inayokatwa kwa mwaka duniani.
“Teknolojia hii tumekwisha kuieneza katika nchi mbalimbali duniani kama vile Nigeria, India na Kenya.
“Tanzania tumeanzia hapa Musoma mkoani Mara… teknolojia hii itawasaidia vikundi vya kina mama ambao wana kazi kubwa za uhitaji wa nishati ya jua,” alisema Lindfors.
Alisema jiko hilo lina uwezo wa kupika vyakula mbalimbali na kukausha karanga, kubani kanyama, kukausha ndizi na kupata unga, kukausha mihogo na mitama na lina uwezo wa kuoka unga wa mikate wenye uzito wa kilo 10.
Monica Macha, mjasiriamali kutoka kikundi cha Alpha Alliance cha Musoma kilichoanza kutumia teknolojia hiyo, alisema kabla ya kutumia jiko hilo walikuwa wanatumia debe moja la mkaa kwa siku katika kuoka mkate au chapati jambo ambalo kwa sasa ni ndoto kwao.