MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Christina Mndeme, amepiga marufuku uingizaji na uchinjaji wa nguruwe, kufuatia mlipuko wa homa ya nguruwe.
Alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na madiwani na watendaji wa Manispaa ya Dodoma.
Alisema hadi sasa zaidi ya nguruwe 200 tayari wameshakufa kutokana na mlipuko huo.
Aliwataka wakazi wa manispaa hiyo kutokula mizoga ya nguruwe ili kuepuka maambukizi ya homa ya nguruwe ambayo kwa asilimia 100 inaua.
Aliwataka kula nyama ya nguruwe iliyopimwa na wataalamu wa afya.
Alisisitiza madiwani kutoa elimu kwa usahihi kwa wananchi wao kuhusu madhara ya mlipuko huo.
Alitaja kata zilizokumbwa na mlipuko huo kuwa ni kata ya Ipagala na Miyuji ambayo zaidi ya nguruwe 200 wameshakufa.
Aliagiza kufanyika doria na kuwakamata watu wote watakaobainika kukaidi amri hiyo.
“Ninawaagiza nyinyi madiwani pamoja na watendaji hakikisheni mnatoa elimu iliyo sahihi kwa uwazi bila kificho, ukizingatia kuwa ugonjwa huu unaua tena kwa asilimia mia moja, hivyo ni marufuku kuingiza ndani ya wilaya hii na wala kuchinja pasiporuhusiwa na wataalamu wa afya,” alisema.
Alisema ingawa ufugaji wa nguruwe ni sehemu ya kujiingizia kipato, kipindi hiki cha mlipuko hakuna sababu ya kupuuza bali wanatakiwa kujiepusha ulaji holela wa nyama hiyo.
Aliwataka wafugaji kujiepusha na uchukuaji wa vyakula vinavyobaki hotelini na sokoni kwa kuwa vinasadikiwa kuwa na vimelea vinavyochangia uwepo kwa homa hiyo.