SIKU moja baada ya wafanyabiashara Harbinder Singh Sethi na James Rugemalira kufikishwa mahakamani na kunyimwa dhamana, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na (Takukuru)-
imesema inaendelea kukamilisha orodha ya watu watakaopandishwa kizimbani kwa tuhuma za kuhusika na uchotwaji wa fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.
Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa Takukuru Makao Makuu, Mussa Misalaba, alisema kwa sasa uchunguzi unaendelea kwa kila aliyehusika, na hatua zitachukuliwa kwa kadri ushahidi utakavyokusanywa.
"Mtu anaweza kutuhumiwa, lakini bila ushahidi huwezi kumshtaki," alisema. "Kama mtu ametuhumiwa na hakuna ushahidi ni vigumu kumkamata ila tunaendelea kukusanya ushahidi na tukijiridhisha tutawakamata.
"Wafanyabiashara waliofikishwa mahakamani ni mwanzo tu, tunaendelea na uchunguzi wetu na kadri tutakapokuwa tunapata ushahidi (watuhumiwa) watahojiwa na kufikishwa kwenye mamlaka husika."
Sethi na Rugemalira walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu juzi wakikabiliwa na makosa mbalimbali, ikiwamo uhujumu uchumi ambayo mahakama hiyo haina mamlaka ya kuyasikiliza hivyo haiwezi kutoa dhamana na washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote.
Wafanyabiashara hao wanakabiliwa na makosa sita likiwamo la kuisababishia serikali hasara ya dola za Marekani 22,198,544.60 (Sh. bilioni 309.4).
MAAZIMIO NANE
Kufikishwa mahakamani kwa wafanyabiashara hao kunaonekana kama mwanzo wa utekelezaji wa maazimio ya Bunge ya miaka mitatu iliyopita.
Mwaka 2014, wakati Bunge likijadili sakata la akaunti ya Tegeta Escrow, lilitoa maazimio nane likiwamo la Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vichukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria dhidi ya watu wote waliotajwa na taarifa maalum ya kamati ya Bunge, kuhusika na vitendo vyote vya jinai kuhusiana na miamala ya akaunti hiyo na watu wengine watakaogundulika kufuatia uchunguzi wa sakata hilo.
Pendekezo la pili la Bunge ni serikali kuangalia uwezekano wa kuichukua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco) kwa mujibu wa sheria za nchi.
Jingine ni kufanya mapitio ya mikataba ya umeme ambalo liliitaka serikali ilitekeleze mapema kwa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wake kabla ya mkutano wa bajeti ya mwaka wa fedha 2015/16.
Bunge pia liliazimia serikali iandae na kuwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria inayounda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi mahususi itakayoshughulikia kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa. Kipindi hicho kulikuwa na Taasisi ya Kuzuia Rushwa (Takukuru).
Chombo hicho cha kutunga sheria pia kiliazimia Rais aunde Tume ya Kijaji ya kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya majaji Aloysius Mujulizi na Jaji Prof. Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Azimio la sita lilikuwa mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi kuitaja Benki ya Stanbic na benki nyingine itakayogundulika kufuatilia uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika akaunti ya Tegeta Escrow kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji fedha haramu.
Bunge pia liliazimia Waziri wa Nishari na Madini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco wakati huo, wawajibishwe kwa kuishauri mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi wao.
Azimio la mwisho ni Kamati za Kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka kwa kuwavua nyadhifa zao kwenye kamati husika viongozi wake waliobainika kukiuka maadili kwa kujihusisha kwa vyovyote vile na uchotaji wa fedha za akaunti hiyo kabla ya kuanza kwa mkutano wa Bunge uliokuwa unafuata.