Nini? Victoria Paschal Kamata ‘Vicky Kamata’ ni Mbunge wa Viti Maalum akiwakilisha Mkoa wa Geita kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), katikati ya wiki iliyopita, aligeuka mbogo na ‘kutoa povu ambalo siyo la nchi hii’ kufuatia swali aliloulizwa na Wikienda juu ya madai ya kufulia, kuuza baadhi ya mali zake ikiwemo lile ghorofa lake kisha kutimkia mkoani Geita kutengeneza makazi mapya.
Habari kutoka kwa chanzo ambacho ni mbunge mmoja ambaye aliwahi kuwa rafiki wa karibu na Vicky, zilieleza kuwa, kwa sasa mwanasiasa huyo ameamua kuuza baadhi ya vitu vyake ikiwemo magari na kujikita kwenye kilimo.
Siku za nyuma, mwandishi wetu aliwahi kuwasiliana na Vicky ambaye alimjuza kuwa yupo mkoani Morogoro ambako anasimamia kilimo cha mazao ya tikiti-maji na kumtania mwandishi amtafutie wateja, jambo ambalo liliishia kwenye vicheko kwani yalikuwa ni mazungumzo ya kawaida.
Kama aya ya kwanza inavyojieleza vyema, baada ya madai ya ‘kulikimbia jiji’, mwandishi alimtafuta tena Vicky na kumtaka afafanue kwa kina juu ya manenomaneno hayo ili kuondoa ukakasi kwani nyuma yake kuna wadau na wapenzi wengi wa kazi zake kama mbunge, msanii na Mkurugenzi wa Taasisi ya Victoria Foundation.
“Unajua wewe (akilitaja jina la mwandishi), mimi na wewe tunafahamiana, tena ni mdogo wangu, sasa mimi nataka nikuulize swali dogo sana, ulipoambiwa maneno hayo, kabla hata ya kunipigia simu na kuniuliza ulipima na kuona kama yanafanana na mimi kweli unayenijua? “Sikutarajia kwa kweli ninavyokuamini kama ungethubutu kuniuliza jambo la kama hilo.
“Hivi unatarajia mimi niolewe na kiongozi mkubwa mwenye wadhifa na maisha yake mazuri (aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Servacius Likwelile) halafu nimhamishe aje nimuoe na kuishi naye nyumbani kwangu?
“Sawa, inaweza kutokea lakini kama sijafanya hivyo? Mambo mengine yanatia hasira sana,” aliwaka Vicky.
Huku akitweta kwa hasira, Vicky aliongeza: “Sikiliza mdogo wangu, kuna watu wanaomba kila kukicha niishiwe na kufilisika, okey, kwani wanaoishiwa si ni binadamu kama mimi? Nenda pale Sinza ukaone Victoria Foundation inavyozidi kufanya kazi.
“Nataka niwaambie hivi, wanaoombea niuze kila kitu, watauza wao na hatimaye kujiuza na wao na Vicky ataendelea kudunda kwa kumtegemea Mungu,” alisema Vicky.