Jana niliona mjadala wa kitoto ulioanzishwa na Mdude Chadema Nyagali Mwanachama wa CHADEMA. Mjadala huo ulianza kwenye Ukurasa wa Facebook wa Mdude Chadema Nyagali na kusambaa kwenye mitandao mingine. Katika mjadala huo ambao aliuita mazungumzo baina yake na dereva wa Bus linalotoka Dar es Salaam hadi Sumbawanga, alijenga hoja kuwa Tozo ya Motor Vehicle iliyopendekezwa kufutwa na Waziri wa Fedha, Philip Mpango ni nafuu zaidi kuliko inayopendekezwa.
Katika mjadala huo, Mdude alifahamishwa na dereva wake kuwa kwa siku anatumia lita 400 kutoka Dar es Salaam hadi Sumbawanga kwa Bus aina ya Yutong. Tena aliupa uzito mjadala huo kwa kuweka picha ya Bus la Shabiby ambalo sina hakika kama linafanya safari hiyo. Kwa maelezo yake, kwa kuwa gari linatumia lita 400, kwa hali hiyo hadi Sumbawanga Busi hilo litalipa motor vehicle ya shilingi 16,000 kwa maana 400 x 40. Kwa Mwezi atalipa Motor Vehicle ya shilingi 16,000 x 30 = 480,000 na kwa mwaka shilingi 480,000 x 12 = 5,760,000.
Mjadala huo ulivuta hisia za wafuasi wa CHADEMA ambao nao bila kutumia akili ipasavyo, wakaanza kushangilia na kujiona wameshinda. Ni kwa bahati mbaya sana Mdude CHADEMA hajawahi kumiliki hata pilipiki kwa hiyo hajui lolote kuhusu consumption ya mafuta kwenye magari. Binafsi nilijiuliza, je umbali wa kutoka Dar es Salaam hadi Sumbawanga unaweza kutumia lita 400? Kama ni hivyo, je abiria wa huko wanalipa nauli kiasi gani? Twende taratibu.
Mabasi mengi yanatumia wastani wa lita moja Diesel kwa kila kilomita 7 hadi . Na kwenye barabara za Highway, consumption ya mafuta ni tofauti na kwenye maeneo ya mijini. Kwa maana hiyo lita 400 anazotuma huyo dereva ukizidisha mara 7 gari hilo litalazimika kutembea kilomita 2800 ili kumaliza mafuta hayo yaani 7 x 400 = 2,800. Je Umbali wa kutoka Sumbawanga hadi Dar es Salaam unafika kilomita hizo?
Haya tufanye gari hilo ni mkweche kiasi cha kutumia kilomita 5 tu kwa lita moja. Maana yake ni kwamba gari hilo litalazimika kutumia kilomita 2000, hadi kumaliza mafuta yote yaani 5 x 400 = 2000. Je umbali wa kutoka Dar es Salaam hadi Sumbawanga unafikia kilomita 2000?
Basi tuseme Tank la Mafuta la Gari hilo linavuja na kwa hali hiyo hutumia lita moja kwa kila kilomita 3 tu. maana yake ni kwamba 3 x400 ni sawa na kilomita 1,200. Je umbali wa kutoka Sumbawanga hadi Dar unafikia kilomita 1,200?
Baada ya kushirikisha ubongo wangu, nilijiuliza maswali haya? Je Mdude Chadema ana uelewa wa matumizi ya mafuta kwenye magari? Au huyo Dereva anampiga cha juu bosi wake na ndo maana akataja kiasi kikubwa cha mafuta?
Ukweli ni kwamba, Motor Vehicle iliyopendekezwa inapunguza sana gharama na hasa kwa sisi tunaoishi huku mikoani. Mathalan, mimi nikijaza full Tank huku Songea natumia wastani wa siku 18 hafi 25 hadi kwenda tena kituo cha mafuta. Kwa maana gari langu aina ya Toyota Harrier ina CC 2160 na ujazo wa Tank ni lita 65. Na inatumia wastani wa kilomita 8 kwa lita moja. Kwa maana hiyo, kwa lita 65 ili ziishe zote ingawa haijawahi kutokea, nitalazimika kutembea kilomita 520 ambayo kwa mzunguko wa mji wetu wa Songea nitatumia wastani wa siku 18 hadi 25 kumaliza na kama ninazurura sana nitatumia siku zisizopungua 10.
Sasa twende taratibu, lita 65 x 40 = shilingi 2,400. Kwa maana hiyo kila siku 15 nitalipa Motor Vehicle ya shilingi 2,400 tu. kwa Mwezi nitalipa shilingi 4,800 tu na kwa mwaka nitalipa shilingi 4800 x 12 = 57,600 tu. hii ni pungufu ukilinganisha na shilingi 200,000 ninayolipa sasa. Yaani nitaokoa shilingi 142,400. Na hapa chukulia kama gari inatembea siku zote. Kama kwa nyakati kadhaa gari halitumiki maana yake ni kwamba kiasi cha Motor Vehicle nitakacholipa kitapungua.
Kwa wale wa Dar es Salaam ambao foleni husababisha matumizi makubwa ya mafuta, twende na mfano huu. Kwa wanaoishi Mbagala, ama Vikindu, ama Kibamba, ama Bunju na wanafanya kazi katikati ya Jiji, hutumia wastani wa lita 70 kwa wiki. Maana yake ni kwamba Motor Vehicle atakayolipa mtu huyo ni kama ifuatavyo; Kwa wiki itakuwa 70 x 40 = 2,800. Kwa mwezi itakuwa 2,800 x 4 = 11,200 na kwa mwaka itakuwa shilingi 11,200 x 12 = 134,400 tu. kwa hali hiyo, mtu mwenye gari kama langu ataokoa shilingi 65,600 kila mwaka iwapo tozo mpya ya Motor Vehicle itapitishwa. Hizi ni hesabu za kitaalam na wewe kama unamiliki gari unaweza kufanya hesabu zako ili kujua utalipa kiasi gani kwa wiki, mwezi na mwaka. Uzuri wa tozo pendekezwa ni kwamba inalipwa kulingana na jinsi unavyolitumia gari lako. Kama weekend una kawaida ya kupumzika basi utaokoa kiasi kikubwa sana cha fedha. Na kama una kawaida ya kupanda daladala siku moja moja ili kuchangamana na jamii kama nifanyavyo mimi basi utaokoa fedha nyingi sana.
Niwasihi Watanzania, tusimezeshwe tu kila kitu. Wengine wanaotumezesha hawajui lolote. Tutumie akili alizotupa Mungu ili kuchanganua mambo.
Nawasilisha
Chanzo JF
Well said, uchambuzi makini.
ReplyDelete