Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Twaweza umebaini kuwa asilimia 71 ya Watanzania wanaukubali utendaji kazi wa Rais John Magufuli ingawa kiwango hicho kimeshuka kutoka asilimia 96 ikilinganishwa na utafiti huo ulipofanyika Juni mwaka jana.
Matokeo haya yametolewa leo Alhamisi na Twaweza katika utafiti wake uitwao ‘Matarajio na matokeo; Vipaumbele, utendaji na siasa nchini Tanzania.’
Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza Aidan Eyakuze, amesema:
“Idadi kubwa ya wananchi inaendelea kuukubali utendaji wa Rais Magufuli. Lakini kushuka kwa viwango vya kukubalika kwake, pamoja na vile vya wabunge, madiwani na wenyeviti wa mitaa, ni ujumbe mzito kutoka kwa wananchi wanaohisi kuwa, tofauti na matarajio yao, wameangushwa na utendaji wa Serikali katika kuzitatua shida zao moja kwa moja. Wananchi wana hofu na vitu vya msingi – kipato na chakula - na wanatuma ujumbe mzito kwa viongozi wao."
"Lakini utafiti unabainisha ujumbe mwingine kutoka kwa wananchi. Katika orodha ya matatizo makubwa matatu yanayowakabili, afya, elimu na maji zimeshuka ngazi,” ameongeza.
Amesema Sekta hizo kwa miaka mitatu mfululizo zilichukua nafasi za juu kama changamoto kuu zilizotajwa na wananchi na hivyo utafiti huu unaashiria kuwa wananchi wanayaona mabadiliko katika upatikanaji wa huduma za jamii.
Utafiti huo unatokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mikononi.
Matokeo hayo yanatokana na takwimu zilizokusanywa Aprili mwaka 2017 kutoka kwa wahojiwa 1,805 katika maeneo mbalimbali Tanzania Bara.
Pamoja na kukubalika kwa Rais Magufuli, lakini kukubalika kwa viongozi wengine kama wabunge, madiwani na wenyeviti wa vijiji na wa mitaa.
Kwa mfano, kukubalika kwa utendaji wa wabunge, kumeshuka kutoka asilimia 79 (Juni 2016) hadi asilimia 58 (Aprili 2017).
Kukubalika kwa utendaji wa madiwani, kumeshuka kutoka asilimia 74 hadi asilimia 59 na kukubalika kwa utendaji wa wenyeviti wa vijiji/mitaa kumeshuka kutoka asilimia 78 hadi asilimia 66.
Kukubalika kwa vyama vya siasa
Kadhalika utafiti huo ulibaini kuwa CCM imeendelea kuimarika kwa kukubalika kwa kati ya asilimia 54 na 64 kati ya mwaka 2012 na 2017.
“Mwaka 2013 na 2014 kiwango cha kukubalika kilishuka na kilifikia asilimia 54 kutoka asilimia 65 ya mwaka 2012. Kukubalika kwa CCM kumeendelea kubaki katika kiwango hicho hicho cha asilimia 62 tangu uchaguzi wa mwaka 2015 na asilimia 63 mwaka 2017,” umesema utafiti huo.
Chadema yaporomoka
Kadhalika utafiti huo umebaini kuwa kukubalika kwa Chadema kumeshuka kutoka asilimia 32 mwaka 2015 hadi asilimia 17 mwaka huu.
Utafiti huo umebaini, CCM inakubalika zaidi miongoni mwa wazee (asilimia 80), ukilinganisha na asilimia 55 ya vijana. Wanawake (asilimia 68) wanaikubali CCM kuliko wanaume (asilimia 58), maeneo ya vijijini (asilimia 66) kuliko maeneo ya mijini (asilimia 57), na wananchi masikini (asilimia 69) kuliko matajiri (asilimia 53).
Wananchi wenye elimu ya sekondari, elimu ya ufundi au elimu ya juu wanaikubali CCM kwa asilimia 46.
Kukubalika kwa Chadema kwa ujumla kunafuata mtiririko tofauti: ni mkubwa miongoni mwa vijana, wanaume, watu matajiri na wenye kiwango kikubwa cha elimu.