Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amesema kamwe Serikali haitagawa chakula kwa wananchi wavivu ambao hawataki kufanya kazi na kusubiri chakula kutoka Serikalini.
Mhe Suluhu ametoa kauli hiyo wakati akihutubia mamia ya wananchi wa Manispaa ya Musoma katika mkutano wa hadhara ambapo amesisitiza kuwa Serikali itapeleka chakula kwa wananchi ambao mazao yao yaliharibiwa kwa mvua au yalikauka kwa ukame au kwa maafa mengine na sio kwa wananchi wanaokaa vijiweni mchana kutwa bila kufanya kazi wakisubiri neema ya chakula kutoka kwa Serikali.
Amewahimiza wananchi kote nchini kuendelea kufanya kazi kwa bidii ikiwemo shughuli za kilimo na pindi wanapovuna wajiwekee akiba na waache tabia ya kuuza mazao yote wanayoyavuna ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa chakula kwenye familia zao.
Aidha Mh. Makamu pia amewataka viongozi wa mkoa wa Mara washirikiane na wananchi katika kuwaelemisha mbinu bora za kilimo ili waweze kupata mazao mengi ikilinganishwa na hali ilivyo kwa sasa.