Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo imesaini mikataba 30 na wakandarasi mbalimbali kwa ajili ya kutekeleza shughuli za miradi ya maendeleo za halmashauri hiyo yenye miezi nane tangu kuanzishwa kwake.
Miongoni mwa miradi hiyo ni uboreshaji miundombinu ya maji na huduma za afya katika Hospitali ya Sinza Palestina na usafi wa barabara za manispaa hiyo.
Mikataba hiyo imesainiwa leo Ijumaa kati ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, John Kayombo, Meya wa manispaa hiyo, Boniface Jacob na baadhi ya wakandarasi.
Halfa ya kusaini mkataba huo imefanyika katika ofisi za makao makuu ya manispaa hiyo zilizopo Kibamba.
Kayombo amewaeleza wanahabari kuwa mikataba hiyo ina thamani ya Sh4 bilioni na utekelezaji wake unatarajiwa kuanza wakati wowote.
Kwa upande wake, Jacob amesema wakarandasi waliopatikana wamefuata sheria na kanuni na hakuna aliyepata tenda kwa njia ya udanganyifu.
"Nikueleze tu mkurugenzi, mtu atakayeshindwa kutekeleza majukumu kwa ufanisi usisite kumchukulia hatua ikiwamo kusistisha mkataba wake,"amesema Jacob.