Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Jumanne Murilo alisema kuwa askari alimkaba Mamla kama njia ya kujihami kutokana na dereva huyo kuelekeza pikipiki mahala tofauti na kituo cha polisi huku akimwambia lazima wafe wote na ndipo askari huyo alipoanza kujihami na kusababisha ajali ambayo kwa bahati mbaya imezua kifo.
SHINYANGA
Mwendesha bodaboda Joel Gabriel Mamla (26) wa Shinyanga mjini alifariki dunia juzi katika ajali iliyotokea katika barabara kuu ya Mwanza -Tabora wakiwa kwenye mwendo kasi kutokana na kukabwa koo na askari polisi PC Edmund, aliyempakia na kuanguka kutoka kwenye pikipiki hiyo na kupasuka kichwa kilipogonga jiwe baada ya kukabwa shingo na polisi huyo alipokamatwa na kuamriwa waende kituoni. Imedaiwa kuwa alifariki dunia baada ya kuanguka kutoka kwenye pikipiki ambayo iligonga nguzo ya barabarani.
Wakisimulia tukio hilo, mashuhuda walisema kuwa waliona mwendesha pikipiki na abiria wake wakivutana mikono na kupigana, hivyo kusababisha pikipiki hiyo iyumbe. Walisema kuwa ilipokaribia eneo hilo la ajali, waliona mwendesha pikipiki huyo akikabwa shingo na abiria na hatimaye kuiachia pikipiki na kuangukia chini. Walipoanguka, ndipo dereva huyo alipiga kichwa kwenye jiwe na kuanza kuvuja damu puani na masikioni.
Mamla alifariki papo hapo na ndipo wananchi wenye hasira wakaanza kumpiga abiria huyo bila kujua ni askari polisi. Wananchi waliendelea kumpiga wakidhani kuwa ni jambazi aliyetaka kupora pikipiki na alinusurika baada ya kukimbilia kwenye nyumba iliyokuwa jirani. Madereva hao waliamua kufanya maandamano ili kufikisha ujumbe Serikalini kuwa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linawaonea. Wanasema kuwa marehemu alikamatwa na askari huyo akiwa amevaa kiraia na bila ya kuonesha kitambulisho na kwamba mazingira haya hayana tofauti na matukio ya unyang’anyi wa pikipiki na ndio maana marehemu hakutii.
Tukio hili limesababisha ugomvi mkubwa kati ya polisi na waendesha bodaboda mkoani Shinyanga, ugomvi uliodumu kwa zaidi ya saa tano na uliisha baada ya polisi kutumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kuwatawanya.
Maandamano haya yalisababisha shughuli zote kusimama mjini Shinyanga kwa muda wote huo wa zaidi ya saa tano.