Kauli hiyo ilitolewa juzi na kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa, Amour Hamad Amour wakati akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Bustani kilichopo katika Halmashauri ya Mji wa Kondoa. Alisema kuna haja ya viongozi kukemea suala la mavazi yasiyofaa kwa wanafunzi hasa ya vyuo vikuu ambayo mengi yamekuwa yakitia aibu.
“Hapa naona ni tofauti kila mmoja kavaa kiheshima, lakini kwenye vyuo vikuu hali ni tofauti mavazi mengi yanayovaliwa yanaleta vishawishi vya ngono na kufanya maisha ya wasichana kuwa hatarini,” alisema.
Pia katika hotuba yake aliwataka wanafunzi kuacha siasa za majitaka na kutafuta njia za kujiletea maendeleo. “Pia mfikirie zaidi kujiajiri hata kwenye kilimo kwani kunalipa, vijana ndio nguvu kazi ya taifa lazima walete mabadiliko lakini ukikaa unaleta siasa chafu, kujihusisha na vikundi viovu, uasherati na matumizi ya dawa za kulevya tutakosa viongozi wazuri wa kuliendeleza taifa,” alisema.
Aliwataka kupiga hatua za kimaendeleo kwani maendeleo ya Watanzania yanatakiwa kuletwa na watu wote. Sambamba na kuzungumza na wanafunzi hao kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge aliweka jiwe la msingi katika ukumbi wa mikutano wa RC Mission. Ukumbi huo utakapomalizika utatumika kwa shughuli mbalimbali za kijamii kama mikutano na makongamano.