Mchanga wa Madini Waendeleza Mvurugano Bungeni..Wabunge Waungana Kutaka Mikataba Yote Ipelekwe Bungeni !!!


Zuio la kusafirisha mchanga wa madini kwenda nje ya nchi liliwagawa wabunge katika mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini uliofanyika wiki hii.

Licha ya wabunge wengi kukubali kwamba Taifa halinufaiki ipasavyo kutokana na uchimbaji wa madini pamoja na rasilimali nyingine zinazoendelea kuvunwa nchini, baadhi ya wabunge, hasa wa upinzani, hawakubaliani na namna mchakato mzima unavyoendeshwa.

Hoja inayotolewa na wapinzani ni ubovu wa sera, sheria na mikataba yote ya madini ambayo mingi haijawekwa wazi hivyo kutolinufaisha Taifa kwa kiasi kilichotarajiwa.

Wapinzani wanataka mchakato wa kufanya marekebisho yoyote uanzie katika mikataba badala ya mchanga ambao ni sehemu ndogo ya kinachopotea.

Akichangia hoja, mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa alisema agizo la Serikali linaweza likawa na athari kwa wawekezaji wa sekta ya madini ambao mitaji yao imeelekezwa huko.

Alikumbusha kwamba wizi wa madini ulielezwa siku nyingi hata ripoti ya baadhi ya tume zilizoundwa zilibainisha mapungufu yaliyomo na kushauri yaliyoelezwa ndiyo yanapaswa kupewa kipaumbele katika mapambano haya.

Mwita Waitara, mbunge wa Ukonga (Chadema), alisema tatizo lililopo ni mikataba ya madini ambayo haijawahi kupelekwa bungeni ili wawakilishi hao wa wananchi waione na kutafuta namna sahihi ya kurekebisha kasoro zilizopo.

Alisema licha ya Rais kuunda kamati ya kuchunguza na wabunge wengi kuguswa na wizi wa madini, bado mjadala unaoendelea unakosa uhalisia kwa sababu kila mmoja anatoa hoja bila kujua mkataba una vifungu vipi vinavyotekelezwa. Alisema kwa kuwa mikataba ilipitishwa na chama tawala ambacho leo kimegundua kuibiwa, “wabunge wanahitaji kuiona mikataba hiyo na kujua mambo mliyokubaliana.”

Wakati wabunge hao wakipendekeza hayo, Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika alisema mwisho wa siku atakayepoteza kwenye vita hivi ni Serikali ambayo italazimika kuilipa Kampuni ya Acacia inayosafirisha mchanga huo fidia kutokana na hasara itakayopata kwa muda wote wa zuio.

Wabunge wengi wa chama tawala wanamuunga mkono Rais kwa hatua hiyo, wakisema ni namna sahihi ya kwenda kwenye mabadiliko ya mikataba iliyosainiwa siku nyingi na wawekezaji waliopo.

Mbunge wa Mbinga Mjini (CCM), Sixtus Mapunda alisema hata kama watakaoathirika na agizo hilo wataenda mahakamani na Serikali ikawa na uhakika wa wizi huo, itashinda kwa kuwa suala hilo halikuwa sehemu ya mkataba.

“Hawatafanya chochote tukiwa na ushahidi. Tume ya kwanza imeonyesha udanganyifu ambao ni kinyume na masharti ya mkataba. Hata wakienda popote tutawashinda. Nampongeza Rais kwa anachokifanya,” alisema.

Msimamo wa Mapunda unafanana na wa Mbunge wa Muheza, Balozi Adadi Rajab ambaye alisema mchakato huo unapaswa kuendelea kwani hakuna kitakachoitisha Serikali.

“Tukiwa na ushahidi, hata tukishtakiwa tutaenda kutoa argument. Tunaibiwa, huo ni ukweli, tunaweza kubishana kwenye kiwango tu,” alisema ambaye kitaaluma ni mwanasheria.

Wabunge kutoka maeneo yenye migodi walitoa ushahidi wa wizi unaofanywa. Mbunge wa Msalala (CCM), Ezekiel Maige alisema suala hilo lilikuwapo anakotoka kiasi cha kuwashawishi wananchi kuyavamia malori yaliyokuwa yanasafirisha mchanga huo na kuuiba.

“Walipochenjua kwa njia za kienyeji, kiroba cha kilo 50 cha mchanga kilitoa mpaka Sh50 milioni. Sasa hivi ulinzi umeimarishwa, malori hayo yanasindikizwa na askari wenye silaha,” alisema Maige ambaye ni mtaalamu wa biashara.

Mbunge wa Geita (CCM), Joseph Msukuma aliwataka wabunge wenzake, bila kujali itikadi kuungana kwenye vita hii kwani jamii zinazozunguka migodi zinafahamu athari za kudumu za wawekezaji wa sekta hii.

“Wametuachia mashimo makubwa. Njooni muyaone. Wameondoka na kila kitu wakati wananchi wanaozungua bado ni masikini na hawana huduma za uhakika za jamii,” alisema Musukuma.

Aliwananga wanaopinga hasa Chadema kwamba wanawatetea wezi hao wa madini ambao kamati imeanika wanachokifanya kwakuwa wamepokea fedha ili wafanye hivyo na wanachokisema kinawaondolea uzalendo mbele ya jamii.

“Nawafahamu waliopewa fedha. Niwataje…niwataje! Semeni basi. Tunajua kuwa mna-retire imprest mlizolipwa,” alisisitiza Musukuma.

Ni suala lililomgusa hata Spika wa Bunge, Job Ndugai aliyesema Bunge lake linaunga mkono hatua alizochukua Rais kukabiliana na jambo hilo kubwa ambalo halifai kufumbiwa macho na akataka kupuuzwa kwa wanaowatetea wezi wa madini. “Hatuwezi kuwa tunaibiwa halafu tunacheka cheka. Hii ni vita kubwa ingawa wapo wat wanaotetea. Unakuta ni mbunge anayetoka sehemu yenye upungufu wa madawati, dawa hospitalini na barabara mbovu. Hii ndiyo namna ya kuwatambua. Mngejuaje sasa? alisema Ndugai akiahirisha kikao cha Bunge Ijumaa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad