Mjue Mgunduzi wa BUNDUKI MAARUFU IITWAYO AK 47

Luteni Jenerali Mikhail Timofeyevich Kalashnikov wa Urusi ndiye mgunduzi wa silaha maarufu sana katika uwanja wa mapambano duniani kote iitwayo AK 47. Ni bunduki iliyobuniwa na kutengenezwa na kamanda huyu wa Jeshi Jekundu (Red Army) la Muungano wa Kisovieti wa Urusi (USSR) wakati huo.

Luteni Jenerali MIKHAIL TIMOFEYEVICH KALASHNIKOV alizaliwa tarehe 10 Novemba 1919 eneo la Kurya, Altai, Urusi, ambalo kwa sasa linajulikana kama Altai Krai, Russia. Alijiunga na jeshi la Urusi mwaka 1938 na kupangiwa kama fundi wa vifaru na baadaye alipanda cheo na kuwa kamanda wa vifaru.

Mwezi Oktoba mwaka 1941 wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, alijeruhiwa vibaya katika mapigano ya Bryansk na kulazwa hospitalini mpaka mwezi Aprili mwaka 1942. Akiwa hospitalini akitibiwa, aliwasikia askari wenzake wa Kirusi wakilalamikia udhaifu wa bunduki zao za Urusi katika uwanja wa mapambano.

Baada ya kubaini udhaifu huo wa bunduki za Urusi, aliamua kutumia ubunifu wake kutengeneza bunduki bora zaidi za jeshi la nchi yake. Baada ya majaribio yake ya muda mrefu, hatimaye juhudi zake zilizaa matunda mwaka 1947 alipofanikiwa kutengeneza bunduki ya AK 47. Jina hili AK 47 ni kifupi cha maneno "Avtomat Kalashnikova model 1947"; namba 47 inasimama badala ya mwaka wa ugunduzi.

Luteni Jenerali MIKHAIL TIMOFEYEVICH KALASHNIKOV alifariki hospitalini tarehe 23 Desemba, 2013 akiwa na umri wa miaka 94 huko Izhevsk, mji mkuu wa jimbo la Udmurtia Urusi.

Huyo ndiye MIKHAIL TIMOFEYEVICH KALASHNIKOV, mgunduzi wa bunduki maarufu kwa jina la AK 47 ["Avtomat Kalashnikova model 1947"].
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad