Mtazamo... Ukitaka Kuaminiwa, Jenga Mazingira ya Kuaminika..!!!!


“Nina mke asiyeniamini kabisa,” aliniambia bwana mmoja hivi majuzi. “Hana imani kabisa na mimi. Juzi kati hapa nimemkuta anachunguza simu yangu. Tuligombana sana.” Nilimwuliza kwa nini anafikiri mke wake hamwamini. “Basi tu ndivyo alivyo. Hata ufanyaje hana imani.”

Sote, kama alivyo bwana huyu, tuna hitaji la kuaminiwa. Tunatamani watu wasiwe na mashaka na sisi. Tunatamani watu waamini yale tunayowaambia.

Pengine nawe, kama huyu bwana umewahi ‘kuwadai’ watu wakuamini. Umekwenda kwa rafiki, mathalani, kumkopa fedha. Rafiki yako anasita. Hakuamini. Kutokuaminiwa kunaumiza hisia kwa sababu, kama tulivyosema, kuaminiwa ni hitaji la kila mtu. Hata mwongo naye anapenda watu wamwamini.

Ufanye nini sasa??? Twende pamoja....

A. Kuaminiwa ni matokeo

Mambo mengi hayaendi bila kuaminiwa. Kazini, wakubwa wa kazi wanapenda mtu anayeaminika. Bila kuaminika, huwezi kupata mafanikio. Mfanyabiashara naye, anapoaminiwa na watu anakuwa kwenye nafasi kubwa ya kupata mafanikio.

Urafiki kati ya watu wawili, hali kadhalika, unategemea kwa kiasi kikubwa namna watu hao wanavyoaminiana. Huwezi kuwa na urafiki mzuri na mtu kama hamuaminiani. Kuaminiwa ni msingi wa mahusiano yoyote ya karibu na hata shughuli zinazohusisha watu zaidi ya mmoja.

Kuaminiwa, hata hivyo, si tukio la siku moja wala haki inayoweza kuidaiwa kwa watu. Mke hawezi kudai ‘aaminiwe’ na mume wake. Mume hali kadhalika. Kuaminika ni zao la tabia zetu. Kuaminiwa ni sawa miamala ya Benki. Unaweza kuchukua kile ulichokiweka. Huwezi kudai zaidi. Fanya mambo matatu uaminiwe.


B. Sema ukweli daima

Fikiria uko mahali na rafiki yako ukamsikia akimdanganya mwenzake kwenye simu. Hata kama aliyedanganywa ni mwingine, kwa vyovyote vile imani yako kwa aliyedanganya inapungua. Uongo unapunguza kuaminika.

Ukitaka kuaminika, jenga tabia ya kusema ukweli. Epuka kusema kitu usichomaanisha kwa lengo tu la kuwafurahisha watu. Usimdanganye mtu hata kama unajua hatagundua. Ukitambulika kama mtu mwenye tabia ya kusema ukweli unawafanya watu wasiwe na wasiwasi na maneno yako. Utaaminika.


C. Timiza ahadi zako

Ni rahisi sana kutoa ahadi hasa kama hujiamini na unatamani kuwaridhisha watu. Hata hivyo, ni vizuri kuelewa kuwa ahadi ni kipimo cha ukomavu wako. Usipotekeleza ahadi zako watu wanakuchukulia kama mtu asiye na ukomavu. Huwezi kuaminika katika mazingira unayoonekana huna ukomavu.

Kuliko kutoa ahadi kwa lengo la kumridhisha mtu, ni bora usiahidi kabisa. Punguza matarajio ya watu kwako, kisha fanya jitihada za kuzidi matarajio hayo. Unapoahidi kufanya kitu, tekeleza. Ukishindwa kutekeleza, kuwa mwuungwana. Omba msamaha. Kwa namna hii watu watakuamini.


D. Heshimu uheshimike

Mtu asiyeheshimika ni vigumu kuaminiwa. Wapo watu wanaaminiwa kirahisi kwa sababu tu wamejijengea taswira ya heshima kwa jamii. Heshima ni zaidi ya vitu ulivyonavyo na namna unavyoonekana. Heshima kubwa unayoweza kupewa na watu inategemea vile unavyowaheshimu. Ukitaka kuheshimiwa, heshimu watu.


Unapokuwa na tabia ya kuwadharau watu; kujiona bora kuliko wengine; watu wanakudharau. Hata wale unaowazidi wanastahili heshima. Hata wanaokukosea na kukutendea mabaya wanastahili heshima. Ukijenga tabia ya kulipa ubaya kwa wema utashangazwa na matokeo.

Jambo la kukumbuka ni kwamba watu wanaweza kupoteza imani na wewe kimya kimya. Si kila mtu anaweza kukutangazia kuwa hana imani na wewe. Linda sana tunda la uaminifu. Imani ikipotea, ni vigumu kuirejesha. 

E. Jifunze kwenda na muda 

Watu wengine wanashindwa kuaminiwa kwa sababu ya kutotunza au kwenda muda ipasavyo. Unaaambiwa uje muda fulani kwa mfano saa 7 kamili mchana wewe unakuja saa 8 kasoro huku ukiwa na sababu lukuki (nyingine zisizo na maana). Hii ni tofauti kabisa na wenzetu wazungu ambao wao huenda na muda kisawasawa (Sijamaanisha waafrika/watanzania wote hatuendi na muda). Kwa taarifa yako ni kuwa watu hupimwa uaminifu kwa uwezo wao wa kutumia muda vizuri.

Habari njema, hata hivyo, ni kwamba kadri unavyojiwekea mazingira ya kuaminika, ndivyo utakavyoendelea kuaminika.

"When you're honest from the beginning you don't have to lie to cover up the lie you already told. Honesty is always the best policy"

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad