Mtoto wa pili wa Kiongozi wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi, Saif al-Islam Gaddafi ameachiwa huru baada ya kuzuiliwa kwa kipindi cha miaka sita.
Saif al-Islam aliyependekezwa na babake kuwa mrithi wake amekuwa akizuiliwa na kundi la wanamgambo wenye itikadi kali Abu Bakr al-Siddiq Battalion katika mji wa Zintan kwa miaka sita. ambaye alitekwa anadaiwa kuachiliwa huru baada ya kupewa msamaha.
Taarifa kutoka mtandao wa Al Jaazera zinasema Wanamgambo hao walimuachilia huru jana Jumamosi ingawaje mpaka sasa bado hajaoneshwa hadharani.
Saif al-Islam Gaddafi alihukumiwa kifo na mahakama mjini Tripoli, magharibi mwa nchi hiyo bila yeye kuwepo mahakamani kwa makosa ya umwagaji damu kwa raia waliokuwa wakiandamana dhidi ya utawala wa baba yake.
Maeneo ya magharibi yanatawaliwa na serikali inayopingana na serikali ya mashariki mwa Libya, lakini serikali hiyo ya magharibi yenye makao yake makuu Tripoli ndiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Awali ziliwahi kuvuja taarifa za uongo kuachiliwa kwake, na wataalam wa masuala ya kidiplomasia na kisiasa wanasema kuachiwa kwake huenda hatua hiyo ikatikisa zaidi hali ya kisiasa na kiusalama nchini Libya.
Saif al-Islam anatafutwa pia na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu, makosa anayodaiwa kuyatekeleza wakati wa juhudi zilizofeli za kujaribu kuzima maasi kabla ya babake kuondolewa madarakani na kuuawa.