MARA: Wiki mbili baada ya aliyekuwa mwalimu wa Shule ya Sekondari Kukirango iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Butiama mkoani Mara, Julius Chacha Marinya (29) kukutwa akiwa amefariki dunia katikati ya barabara eneo la Baruti Musoma Mjini, mkewe Mukomkama Rwechungura amefunguka mazito juu ya kifo cha mumewe.
Mwanamke huyo ambaye ni mwalimu katika Shule ya Msingi Nyamisisi iliyopo pia katika Halmashauri ya Butiama, amesema kwamba, tangu aolewe na mumewe huyo mwaka 2013 na kufunga ndoa ya Kikristo kwenye Kanisa Katoliki walikuwa wakiishi vizuri katika ndoa yao hadi mwanzoni mwa mwaka huu mumewe alipoamua kuasi ndoa yao na kumchukua mke wa mtu na kumhamishia Musoma kutoka Kiabakari.
Mwalimu Mukomkama amefafanua kuwa, mara baada ya mumewe kufanya mapenzi na mwanamke huyo ambaye ni nesi (jina tunalihifadhi) wilayani Butiama, mumewe alibadilika ghafla na kuhama nyumbani kwake kwa kumhamisha mwanamke huyo kwenda Musoma kutoka Kiabakari licha ya kuendelea kufanyia kazi Butiama ambapo amesema mbaya zaidi ni kwamba kila siku za kazi mumewe akiwa amelala nyumbani kwake alikuwa akimfuata asubuhi nesi huyo kutoka Musoma kwenda kazini, baada ya kazi jioni alimrudisha tena Musoma.
“Nilipokuwa nikimsihi aache mambo ya mwanamke huyo ili tulinde ndoa yetu kama tulivyoapa siku ya kufunga ndoa, alikuwa akinijia juu na kunipiga na mabapa ya mapanga na kunitishia kuwa
kama ningeendelea kumfuatilia angeniua,” alisema mwalimu huyo kwa huzuni huku akitokwa na machozi.
Aidha, alilieleza Uwazi kwamba, mapema mwezi uliopita alijaribu kumbembeleza mumewe akae nyumbani, atulie walee watoto wao lakini cha kushangaza alimpiga kwa mabapa ya panga kisha akavua pete ya ndoa na kuirusha chini akiashiria kuwa hamtambui tena kuwa ni mkewe na kwenda kwa huyo hawara yake.
“Chanzo cha kifo cha mume wangu naamini kuwa ni huyo mwanamke kwani bila yeye mume wangu asingetangatanga kwenda Musoma,” alisema kwa masikitiko Mukomkama na kuongeza kuwa;
“Hata kabla ya mume wangu hajakutwa na mauti aliondoka hapa nyumbani Mei 12 bila kuaga na hakurejea hadi mwili wake ulipokutwa barabarani Mei 14, mwaka huu saa 2.00 usiku,” alisema.
Mjane huyo aliongeza kuwa, kufuatia mgogoro huo wa ndoa aliondoka nyumbani kwake kwa siku kadhaa kwa hasira, lakini alirudi kwa ajili ya kulinda nyumba.
Mwili wa Mwalimu Chacha uliokotwa barabarani eneo la Baruti Musoma mjini Mei 14, saa 2.00 usiku pembeni kukiwa na pikipiki yake na baadaye alitambuliwa baada ya picha yake kurushwa kwenye mitandao ya kijamii.