BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte) limeagiza wanafunzi wa astashahada na stashahada kuomba udahili moja kwa moja kwenye vyuo wanavyotaka kusoma.
Nacte imewataka wanafunzi hao kuachana na mfumo wa kielektroniki wa baraza hilo na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), ambao walikuwa wakiutumia kuomba nafasi hizo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyobandikwa kwenye tovuti ya Nacte, wanafunzi hao ni wanaoomba kusoma kozi mbalimbali kwa mwaka wa masomo 2017/18.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa uombaji huo hautahusu kozi za afya na ualimu zinazotolewa na vyuo vya serikali pekee.
Uamuzi wa Nacte umetolewa siku chache tangu TCU nayo itangaze wanafunzi wote wanaotaka kujiunga na vyuo vikuu kwa mwaka wa masomo 2017/2018 watatumia mfumo mpya ambao unawataka kwenda vyuoni moja kwa moja kuomba nafasi.
TCU iliwataka wanafunzi waliomaliza kidato cha sita kwa mwaka wa masomo 2016/2017 kuomba nafasi ya kujiunga na vyuo vikuu moja kwa moja vyuoni kuanzia Julai 22 mpaka Agosti 13.
Hatua za Nacte na TCU zimekuja wiki chache tangu Rais John Magufuli akosoe mfumo wa udahili wa wanafunzi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mabweni mapya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Aprili 15, Rais Magufuli alisema utaratibu wa sasa unawachanganya wanafunzi.
“Ninaamini kama wanafunzi wangepewe nafasi ya kuchagua vyuo wanavyovipenda wenyewe, vyuo vya serikali kama vile UDSM, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine na Chuo Kikuu cha Mzumbe vingekuwa na wanafunzi wengi sana,” alisema.
MOJA KWA MOJA
Taarifa ya Nacte ambayo imetolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, ilieleza “Baraza linapenda kuwataarifu wadau wa sekta ya Mafunzo ya Ufundi na Umma kwa ujumla kuwa udahili na uchaguzi wa wanafunzi kwa ajili ya masomo ya Astashahada na Stashahada mbalimbali yanayotolewa na vyuo vyote hapa nchini, utafanyika moja kwa moja vyuoni.”
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa udahili wa kozi za Afya na Ualimu katika vyuo vya Serikali utaratibiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Baraza (NACTE).
Aidha, imeelekeza maombi ya udahili kwa kozi za Afya na Ualimu kwa vyuo vya serikali yatatakiwa kutumwa kwa njia ya mtandao kupitia tovuti ya Nacte au kupitia vyuo husika vya Afya na Ualimu ambavyo vitashughulikia maombi hayo na kufanya udahili kwa njia ya mtandao.
Kabla ya maoni ya Rais Magufuli, wanafunzi wa elimu ya juu walitakiwa kuomba kupitia nafasi vyuoni kupitia Nacte na TCU, ambazo zilichagua wenye sifa za kujiunga na masomo ya vyuo husika.