Akitoa hukumu hiyo jana Ijumaa, Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa amesema endapo mshtakiwa huyo atashindwa kulipa kiasi hicho cha fedha atatumikia kifungo cha miaka mitano jela.
Hukumu hiyo ya shtaka la sita la kutakatisha fedha ilitolewa baada ya Wakili wa Serikali, Christopher Msigwa kumsomea maelezo ya awali (PH) Ndama na kuyakubali maelezo yote yanayounda shtaka hilo la kutakatisha fedha, akapatikana na hatiani na kupewa adhabu hiyo.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili Msigwa aliiambia Mahakama kuwa mshtakiwa amekubali shtaka la sita la kutakatisha fedha na maelezo yanayounda shtaka hilo.
“Hatuna kumbukumbu za nyuma za makosa dhidi ya Ndama ila ni rai ya upande wa mashtaka kuwa wakati mahakama ikitoa adhabu izingatie matakwa ya kifungu cha 13(a) cha sheria ya kuzuia utakatishaji fedha,” imesema hati ya hukumu.
Alisema pia mahakama ibebe dhana ya sheria hiyo ambayo lengo lake ni kuzuia makosa ambayo yanalenga kudidimiza uchumi wa nchi na uzito wa kosa ambalo mshtakiwa amelifanya.
Kwa upande wa Wakili Wabeya Kung’e anayemtetea mshtakiwa huyo kwa kushirikiana na Jeremiah Mtobesya, Kung’e aliiambia mahakama kuwa ni wazi mshtakiwa amekiri kosa baada ya kusomewa maelezo ya awali hivyo mahakama isitoe adhabu kali kwa mshtakiwa.
Aliiomba mahakama izingatie maombi yao kwa sababu mshtakiwa huyo hilo ndiyo kosa lake la kwanza, kitendo chake cha kukiri kosa kinaonyesha kusikitikia kosa alilolitenda na kwamba anayo familia ambayo inamtegemea ambao kwa kipindi cha mwaka mmoja ambacho amekaa ndani imepata shida kwa kukosa huduma yake.
“Kwa kuzingatia kifungu cha 13(a) cha sheria ya kutakatisha fedha ni rai yetu mahakama tukufu isitoe adhabu kali kwa mshtakiwa kwa sababu amejutia kosa alilolitenda,” alisisitiza Kung’e. Hivyo Ndama alihukumiwa kulipa faini ya Sh 200 milioni ama akishindwa kutumikia kifungo cha miaka mitano jela.
Juni 6, 2017 Ndama aliiomba mahakama akumbushwe shtaka, akakumbushwa na Wakili wa Serikali, Esterzia Wilson na akalikubali shtaka hilo.
Akisomewa maelezo ya awali mahakamani hapo, Ndama alikubali maelezo ya awali aliyosomewa ikiwamo nyaraka zilizotumika kufungua akaunti iliyotumika kuingizwa fedha hizo, hundi 18 zilizotumika kutolea fedha hizo, maelezo ya benki ‘bank statement’ na Swift massage.
Iwapo atakamilisha kulipa Sh200 milioni atakuwa huru kuendelea katika mashtaka matano mengine yanayomkabili mahakamani hapo ambayo upelelezi wake bado haujakamilika.
Ndama anatakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika na atoe fedha taslimu kiasi cha Dola za Marekani 270,200 ambacho ni sawa na zaidi ya Sh600 milioni mahakamani hapo na mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.