Pamoja na Kuwa Katika Muungano wa Kivyama ..Odinga, Musyoka Watofautiana Upigaji Kampeni..Kila Mmoja Awataka Wakenya Wachague Chama Chake!!!


Mgombea urais kupitia muungano wa Nasa, Raila Odinga ametofautiana hadharani na mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka kuhusu upigaji kura kwa vyama sita katika uchaguzi mkuu ujao.

Wakizungumza wakati wa Futari iliyoandaliwa na Gavana wa Mombasa, Hassan Joho juzi, Musyoka aliwataka wafuasi wa chama cha ODM waache kuwapigia kampeni wagombea wao tu kwani hiyo itasababisha kukosekana usawa.

“Msishangilie ODM, ODM ODM na badala yake chukueni kila kitu kwa sababu vinginevyo tutabaki bila kitu,” alisema Musyoka.

Aliongeza, “Katika ushirikiano wetu kuna chama cha Amani National Congress na vingine ndani ya Nasa. Hebu tuache kuwaambia wapigakura wachague wagombea wa ODM pekee.”

Lakini ilipofika zamu ya Odinga kuzungumza, aliwataka wapigakura kuchagua wagombea wa ODM akisema hata kama wote wako kwenye muungano, kila chama kinapiga ngoma ili wagombea wake wachaguliwe.

“Nafahamu kwamba Musyoka atapiga kampeni kwa ajili ya chama chake cha Wiper, Musalia Mudavadi atapigia debe ANC, Moses Wetangula Ford-Kenya na Isaac Ruto ataomba mbinu zifunguke ili mvua inyeshe mazao ya Chama Cha Mashinani yakue. Lakini ninasema wachagueni wagombea wa ODM hapa Mombasa,” alisema Odinga.

Wagombea hao waliwahimiza wapigakura kuchagua wagombea kutoka muungano wa Nasa ili waweze kuiondoa madarakani serikali ya Jubilee Agosti 8.

“Serikali hii, kuliko nyingine yoyote imewatesa Waislamu. Mpaka leo hawajulikani walipo baadhi ya vijana wa Kiislamu na mashehe na sisi Waislamu tunatendewa kama raia wa daraja la chini,” alisema Joho.

Odinga, Musyoka, Mudavadi, James Orengo, Joho na wabunge Junet Mohamed (Suna Mashariki), Abdulkadir Mohamed (Mbalambala), naibu spika wa zamani wa Bunge Farah Maalim na Abdulswamad Nassir (Mvita) wote waliilaani serikali ya Jubilee kwa mauaji ya siri ya Waislamu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad