Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye yuko kwenye mgogoro na chama chake cha CUF, amesema kama hasimu wake, Maalim Seif Sharif Hamad atamwalika kwenye sikukuu ya Idd el Fitr, atahudhuria kwa kuwa hana tatizo naye.
Profesa Lipumba alisema hayo juzi alipozungumza na mwandishi wetu wakati wa futari iliyoandaliwa na mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi.
“Sina tatizo na mtu yeyote,” alisema Profesa Lipumba alipoulizwa kuhusu kuwa pamoja na katibu huyo mkuu wa CUF wakati huu wa siku kuu.
Alisema viongozi wa dini waliokuwapo katika hafla hiyo ya futari walihubiri suala la umoja ambalo linatakiwa kuzingatiwa pia hata kwenye vyama vya siasa.
Alisema mafundisho hayo ya viongozi wa dini yalilenga kuwepo kwa umoja, suluhu na mshikamano na kuwasihi viongozi wa CUF kuwasikiliza viongozi wa dini ili kutafuta suluhu.
“Sisi CUF ni moja, kama mtu aliteleza ni aliteleza tu. Nawakaribisha tuje tujenge chama chetu chenye guvu kitakachosimamia upatikanaji wa haki sawa kwa wananchi wote, sina matatizo na mtu yeyote,” alisema Profesa Lipumba.
Profesa Lipumba aliingia kwenye mgogoro na CUF baada ya kujiuzuru uenyekiti mwaka 2015 na kubatilisha uamuzi huo mwaka mmoja baadaye, jambo ambalo lilikataliwa na Mkutano Mkuu.
Lakini Lipumba aliwataka wanachama wanaompinga kujirudi na kujua makosa yao ili kukaa pamoja na kukijenga upya chama na kuahidi kuwa hatakuwa na tatizo na mtu ambaye atafanya hivyo.
Wiki iliyopita, Maalim Seif, akiwa katika hafla kama hiyo ya futari iliyoandaliwa nyumbani kwa mbunge wa Temeke (CUF), Abdalah Mtolea, alisema chama hicho hakimtambui Profesa Lipumba kama mwanachama wake na kwamba mwisho wa mwenyekiti huyo kisiasa umekaribia.
Maalim alidai kuwa Profesa Lipumba amewekwa kwenye nafasi hiyo na dola ili kuhakikisha ushindi wa urais haupatikani na chama hicho kinadhoofika.