PROF. Muhongo Afunguka Uhusika Wake Katika Mikataba ya MADINI, Kutokuwapo Kwake Bungeni Kipindi Cha BUNGE la Bajeti

Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo amesema hahusiki na mikataba ya yote ya madini.

Muhongo alitoa maelezo hayo jana, ikiwa si siku moja baada ya Nipashe kuripoti kutoonekana kwake bungeni bila ruhusa ya Spika.

Aidha, Prof. Muhongo alidokeza Nipashe chanzo cha kutokuwapo kwake katika chombo hicho cha kutunga sheria kwa wiki tano sasa.

Gazeti hili jana liliripoti kuhusu kutoonekana bungeni kwa mbunge huyo wa Musoma Vijijini (CCM) bila ruhusa ya Spika tangu uteuzi wake katika baraza la mawaziri utenguliwe wiki tano zilizopita.

Katika ripoti hiyo ya jana, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alisema ofisi yake haina taarifa za mtaalamu huyo wa kimataifa wa Jiolojia na haijui aliko tangu alipoachishwa nafasi ya uwaziri, muda mfupi baada ya Rais John Magufuli kukabidhiwa ripoti ya Kamati ya kwanza ya uchunguzi wa mchanga wa dhahabu (Makinikia) Mei 24, mwaka huu.

Hata hivyo jana asubuhi Prof. Muhongo kupitia simu yake ya mkononi ambayo kwa siku tofauti amekuwa akipigiwa bila kupokea, alituma ujumbe mfupi wa maandishi kwa Nipashe akikana kuhusika na mkataba wowote wa madini na kutolea ufafanuzi kutokuwapo kwake bungeni kipindi hiki muhimu cha Bunge la bajeti.

Katika maelezo yake Prof. Muhongo alisema hahudhurii vikao vya Bunge kwa kuwa yuko mapumziko.

Aliongeza kuwa kipindi hiki hataki malumbano na hahusiki na mikataba mibovu ya madini ambayo kwa sasa 'imeteka' vinywa vya watanzania wengi wakiwamo wabunge.

"Muhongo yuko mapumzikoni. Hataki malumbano na hahusiki na mikataba yote hiyo", aliandika.

Nipashe ilipotaka kujua mahali ambapo Prof. Muhongo ameamua kupatumia kupumzika, msomi huyo alijibu kwa ufupi " It is my private life''(ni maisha yangu binafsi).

Nipashe pia ilitaka kujua kauli ya Prof. Muhongo kuhusu kutenguliwa kwa uwaziri wake na sababu za kuamua kwenda mapumzikoni kipindi hiki ambacho Bunge linajadili bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha.

Hata hivyo, msomi huyo hakuwa tayari kueleza kwa kina. Katika majibu yake Prof. Muhongo aliandika: " Tuheshimu taratibu za malezi, utamaduni, uzoefu na tabia ya kila mmoja wetu".

Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah aliiambia Nipashe juzi kuwa ofisi yake haina taarifa za Muhongo jambo ambalo ni kinyume na utaratibu.

Chanzo: Nipashe

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad