MWANATAALUMA kutoka nchini Kenya, Profesa Patrick Lumumba amesema kuwa endapo Rais John Magufuli ataendelea na jitihada za kupambana na ufisadi kwa miaka 10, uchumi wa Tanzania utakuwa juu.
Profesa Lumumba alisema jana kwenye Tamasha la Tisa la Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alipokuwa akizungumzia mwanasiasa kuinuka na kuanguka barani Afrika.
Katika maelezo yake, Profesa Lumumba alisema rushwa imeondoa afya barani Afrika, wanasiasa wanapoiacha ikawatawala inawaletea shida. Alisema kwa kipindi kifupi Rais Magufuli alipoingia madarakani, ameonesha njia kwa wanasiasa wengine barani Afrika, ambao wamekumbatia rushwa na kuwaacha wananchi.
“Magufuli ana pumzi ya hewa safi, kama ataendelea hivi baada ya miaka 10 uchumi wa Tanzania utakua juu. Mungu msaidie Rais John Magufuli,” alisema Profesa huyo. Kwa upande mwingine, alisema kuwa Afrika ni bara zuri na lenye uwezo, ila kilichofanyika kwa miaka 30 iliyopita kumekuwa na viongozi wabinafsi, lakini katika miaka ya sasa wameibuka viongozi wazalendo kama Magufuli, Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais Yoweri Museveni na wengineo.
“Viongozi kama hawa wakiungwa mkono na wananchi wazalendo, Afrika itapiga hatua,” alisema. Aliwataka waafrika wajue watambue kuwa umoja ni nguvu utengano ni udhaifu, hivyo ni jambo linalochukua muda mrefu. “Ni jambo lililonifurahisha kuwa Magufuli ametoa mafichoni watu waliohodhi mali zetu kwa muda mrefu na kukubali kulipa. Ni hatua nzuri inastahili kupongezwa,” alisema.