Rais Magufuli Kushusha Panga Jipya Mchanga wa Dhahabu

Rais Magufuli
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli, leo anapokea ripoti ya kamati ya pili aliyoiunda kufuatilia athari za kiuchumi na za kisheria kuhusiana na usafirishwaji wa mchanga wa dhahabu kwenda ughaibuni.

Aidha, wakati Rais akitarajia kukabidhiwa ripoti hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam na tukio hilo kurushwa moja kwa moja kupitia matangazo ya luninga, kuna taarifa kuwa baadhi ya viongozi katika mamlaka mbalimbali zinazohusika na suala hilo wameingiwa na hofu kwa kujua kuwa wanaweza kuchukuliwa hatua ya kutumbuliwa endapo itabainika kuwa kuna kasoro katika usimamiaji wa suala hilo, kama ilivyotokea kwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo.

Ripoti atakayokabidhiwa Rais Magufuli kesho kuhusiana na suala la mchanga wa dhahabu (makinikia) ni ya pili, ikiwa ni baada ya kupokea ripoti ya awali ya kamati iliyohusisha wataalamu nane wa masuala ya madini, wakiongozwa na mwenyekiti wake, Prof. Abdulkarim Mruma.

Magufuli alitangaza kumuondoa Muhongo katika uwaziri na pia kuwaondoa viongozi kadhaa wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) baada ya ripoti kubaini kuwapo kwa tofauti kubwa kati ya kiwango kinachoripotiwa na uhalisia wa kile kilichomo katika makontena 277 ya mchanga wa madini yanayoshikiliwa katika Bandari ya Dar es Salaam na maeneo mengine nchini ambako yalikuwa tayari kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ilieleza kuwa Rais Magufuli atapokea taarifa ya kamati ya pili ya wachumi na wanasheria iliyofanya uchunguzi wa madini yaliyomo kwenye makontena hayo ya mchanga wa madini.

“Tukio hili litarushwa hewani moja kwa moja (mubashara) kupitia vyombo mbalimbali vya habari vya redio, televisheni, mitandao ya kijamii na tovuti rasmi ya Ikulu ambayo ni www.ikulu.go.tz, kuanzia saa 3:30 asubuhi,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa.

Wakati wa kuundwa kwa kamati hiyo ya pili ya wanasheria na wachumi Aprili 10, mwaka huu, Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu, Balozi John Kijazi, aliwataja wajumbe wake kuwa ni ni Prof. Nehemiah Osoro, Prof. Longinus Rutasitara, Dk Oswald Mashindano, Gabriel Malata, Casmir Kyuki, Butamo Philip, Andrew Massawe na Usaje Usubisye.

RIPOTI KAMATI YA WATAALAMU Katika ripoti ya kamati ya wataalamu wa madini iliyokabidhiwa kwa Rais Magufuli, Jumatano ya Mei 23, mwaka huu, ilibainika kuwa taifa limekuwa likipoteza mapato makubwa kupitia usafirishaji wa mchanga wa madini.

Akiwasilisha ripoti hiyo kwa Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam, Prof. Mruma, alisema kuwa kwa ujumla, thamani ya madini yote katika makinikia kwenye makontena 277 yaliyozuiliwa ni Sh. bilioni 829.4 kwa kutumia viwango vya wastani na Sh. trilioni 1.44 kwa kutumia viwango vya juu.

Kwa mujibu wa kamati, kiasi hicho cha fedha ni jumla ya thamani ya madini ya dhahabu, shaba na madini mengine ya metali mkakati (strategic metals) yakiwamo ya Sulfur, chuma, Iridium, Rhodium, Ytterbium, Beryllium, Tantalum na Lithium.

Mbali na Mruma, wajumbe wengine wa kamati ya kwanza ya wataalamu walikuwa ni Prof. Justianian Ikingula, Prof. Joseph Bushweshaiga, Dk. Yusuf Ngenya, Dk. Joseph Philip, Dk. Ambrose Itika, Mohamed Makongoro na Hery Gombela.

HOFU YA PANGA JINGINE Baada ya kupokea ripoti ya kamati teule ya wataalamu, ndipo Rais Magufuli alipotengua uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Muhongo na kuviagiza vyombo vya ulinzi na usalama viwachunguze na ikiwezekana wachukulie hatua watumishi waliokuwa wakihusika kubariki usafirishaji wa mchanga huo wa dhahabu, kuanzia Kamishna wa Madini aliyepita, watumishi wa Wakala wa Ukaguzi wa  Madini (TMAA) na kila mmoja.

Uamuzi huo wa Rais Magufuli utokanao na ripoti ya kamati ya wataalamu unatajwa kuwa ndiyo chanzo cha kuwapo hofu, baadhi wakijua kuwa ripoti ya wachumi na wanasheria inaweza pia kuwaondoa kwenye nafasi zao ikiwa itabainika kuwa kuna mahala walihusika kufanya uzembe.

“Wapo wakubwa hivi sasa hawana raha. Hofu imewajaa kwa kujua kuwa Rais hana simile katika suala hili lenye maslahi makubwa kwa taifa,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe kwa sharti la kutotajwa jina.

Hata hivyo, Nipashe haikuweza kuthibitisha kupitia vyanzo vingine huru juu ya kuwapo kwa vigogo wenye hofu ya kuondolewa kwenye nafasi zao kesho.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Kama ulilima michongoma basi ndio ukalie sasa vx zitakua zauchungu tunataka kuona mfano kwa waliofanya mcheo huu

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad