Kwa mara ya kwanza, mkuu mpya wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Elisha Mghwira amezungumzia na kuweka wazi mazingira yote ya utezi wake ambapo pamoja na mambo mengine, amesema kuwa, wakati akiteuliwa, hakuwa nchini hivyo hakuwa na taarifa za uteuzi wake na kwamba hakuwa hewani kimawasiliano, jambo ambalo lilimpa mshangao mkubwa.
Katika mazungumzo na Uwazi kwa njia ya simu jana jioni, Mama Mghwira ambaye alikuwa Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha ACT-Wazalendo alisema alikuwa nje ya nchi kwa kazi zake binafsi ambapo alirejea juzi (Jumapili) usiku na kukutana na habari za uteuzi huo.
Mghwira: Kwanza sikuwepo nchini wakati wa uteuzi, nimerejea jana (juzi) usiku na kukutana na habari hizo nje ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia).
Uwazi: Kwani hakukuwa na mawasiliano kwa njia ya simu kutoka mamlaka ya uteuzi?
Mghwira: Sikuwa hewani kwa muda mrefu, simu yangu iliibwa na mtu akawa anatumia namba yangu, hivyo watu wa mtandao wakaifunga, nimeirejesha leo tu na wewe ni miongoni mwa watu wa mwanzo kabisa kunipigia.
Uwazi: Kwa hiyo hujapokea taarifa rasmi kutoka mamlaka ya uteuzi?
Mghwira: Taarifa rasmi niliziona kwenye barua kupitia mitandaoni na kama nilivyokueleza, nimewasili jana usiku, sijafanya chochote na hata wao hawajui kama nipo na nawatafuta muda si mrefu kuanzia sasa.
Uwazi: Sasa utajigawaje kikazi? Mkuu wa mkoa ni serikali na wewe uko chama cha upinzani?
Mghwira: Kwani upinzani ni nini? Nadhani muhimu ni kuleta maendeleo katika jamii, lakini tutakaa na kutoa tamko rasmi la chama.