Rais John Magufuli, Jumatatu atapokea taarifa ya kamati ya pili ya wachumi na wanasheria iliyofanya uchunguzi wa madini yaliyo kwenye makontena yenye mchanga wa madini (makinikia) yaliyopo katika maeneo mbalimbali nchini.
Taarifa iliyotolewa leo (Jumamosi) na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa imesema tukio hilo litarushwa hewani moja kwa moja kupitia redio, televisheni, mitandao ya kijamii na tovuti rasmi ya Ikulu ambayo ni www.ikulu.go.tz kuanzia saa 3:30 asubuhi.
Ikulu imewakaribisha wananchi kufuatilia matangazo hayo kupitia vyombo hivyo au simu za mkononi kwa kutembelea tovuti hiyo.
Mei 24, Rais Magufuli alipokea ripoti ya kamati ya kwanza yenye wajumbe wanane iliyochunguza aina na viwango vya madini yaliyomo kwenye mchanga wa madini uliomo ndani ya makontena yaliyozuiliwa na Serikali kusafirishwa nje ya nchi.
Kamati hiyo aliiteua Machi 29, mwaka huu ikiwa na wajumbe ambao ni wana taaluma katika fani za jiolojia, kemia, uhandisi kemikali na uhandisi uchenjuaji madini.
Baada ya kuipokea ripoti hiyo, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Rais Magufuli pia aliivunja Bodi ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na kumsimamisha kazi mkurugenzi mtendaji wake.