Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema ripoti ya uchunguzi wa utata wa watoto pacha ambao mmoja anadaiwa kuibwa katika Hospitali ya Temeke imebaini kuwa, mama huyo Asma Juma alikuwa na mimba ya mtoto mmoja.
Akitoa ufafanuzi wa ripoti ya uchunguzi huo, leo (Ijumaa) Mwenyekiti wa Kamati ya Uchunguzi huo, Profesa Charles Majinge amesema kuwa inawezekana kuna makosa yalitokea katika vipimo vya utrasound na kwamba hata wataalam wa hospitali ya Temeke, walifanya makosa kwa kumfanyia huduma ya upasuaji bila kumfanyia vipimo zaidi vya ultrasound.
Pia Profesa Majinge alisema kuwa hapakuwa na sababu ya mama huyo, Asma Juma kuandikiwa kufanyiwa upasuaji wa dharura ingawa hakufanyiwa huduma hiyo ya dharura.
Kabla ya kutoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari, Waziri Mwalimu na Profesa Majinge walikutana na familia ya Asma na kuwapatia matokeo ya ripoti, matokeo ambayo hata hivyo yamemfanya mama huyo kuangua kilio.