Serikali Yaingizwa Hasara Zaidi ya Bil 20

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeingizwa hasara zaidi ya Bilioni 20 kwa kipindi cha mwaka mmoja uliyopita kutokana na bidhaa bandia na zisizokuwa na viwango (feki) zinazoingizwa nchini.
 
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Kilimo na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti maalumu Shai Joseph Raymond alipotaka kujua ni hasara gani imepatikana kwa mwaka mmoja uliyopita kutokana na bidhaa bandia na zisizokuwa na viwango zinazoingizwa nchini zikiwemo Pembejeo za kilimo, dawa za mifugo, dawa za binaadamu, vyakula, vinywaji, vifaa vya majumbani n.k.

"Katika kipindi cha Januari hadi Decemba mwaka 2016, Tume ya Ushindani ilikamata bidhaa bandia zenye thamani ya shilingi Bilioni 18.67, bidhaa hizo zilikamatwa kwenye kaguzi za bandarini, vitengo vya makontena na katika masoko. Kipindi cha Julai 2016 hadi Marchi 2017 Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa kushirikiana na taasisi nyingine waliteketeza bidhaa mbalimbali zenye thamani ya shilingi Bilioni 2.4 bidhaa hizo ni pamoja na nguo, nyama na soseji, vilainishi vya injini, betri za magari na sola 1430" alisema Mhandisi Kamwelwe

Vile vile, Mhandisi Kamwelwe amesema Shirika pia liliweza kufanya ukaguzi wa mabati na kuteketeza 84000 ambayo hayakuweza kukidhi viwango.

Pamoja na hayo, Mhandisi Kamwelwe amesema serikali kupitia tume ya ushindani (FCC) pamoja na kushirikiana wamiliki wa nembo za biashara inaendelea kudhibiti biashara bandia zisiingie nchini ili kufanikisha ushindani wa haki katika biashara.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad