Serikali Yapigilia Msumari Vyeti Feki...Wavivu Kazini Ofisi za Serikali Nao Kukiona Cha Moto

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki, alisema hayo jana akifanya majumuisho ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018.

Waziri Kairuki alisema kumekuwa na maneno maneno kuwa wizara hiyo imekuwa ikitumia muda mwingi kuhakiki na kuangalia wenye vyeti feki hali ambayo imekwamisha majukumu mengine.

“Baadhi ya watu wanalalamika kuwa tunatumia muda mrefu, sasa nasema tutaendelea kuhakiki na wala hakutakuwa na ukomo.

Tuko tayari kuitwa wizara ya uhakiki, lakini hatuwezi kuacha wakati kazi hiyo imeonyesha mafanikio makubwa, na tumegundua zaidi ya watumishi hewa 10,000 ambao walikuwa wakitugharimu Sh. bilioni 20 kila mwezi. Sasa kwa nini tusiendelee kuwatafuta?” Alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki, alisema kuanzia Julai Mosi, mwaka huu, serikali itaanza kuwafanyia tathmini ya kazi watumishi wake (perfomance audit) ili kubaini wanaofanya kazi na wale ambao wamekuwa wakifanya kwa mazoea.

Alisema mifumo yote ya kusimamia utaratibu huo imeshashughulikiwa na imekamilika, hivyo watumishi wote wa umma watambue kuwa kuanzia tarehe hiyo watakuwa wakifanyiwa tathmini ya kazi zao.

Kuhusu maneno yanayosemwa mitaani kuwa serikali imesitisha ajira, Waziri Kairuki alisema serikali inaendelea kuajiri kwenye maeneo mbalimbali na kwamba itakuwa ikifanya hivyo awamu kwa awamu.

“Niwatoe hofu wahitimu kwamba wawe watulivu tu na ajira zipo na zinaendelea kutolewa kwa kada mbalimbali, tumeshatangaza ajira 52,000 kwenye Bajeti hii na watumishi 9,000 tayari wameajiriwa,” alisema Waziri.

Aidha, alisema serikali itaendelea kupambana na wezi wa rasilimali za umma na aliwaomba Watanzania kuendelea kuipa ushirikiano serikali ya awamu ya tano.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad