KAMPUNI ya bahati nasibu ya SportPesa imesema inafikiria uwezekano wa Simba na Yanga kucheza mechi dhidi ya timu ya Everton inayocheza Ligi Kuu England ili kutoa fursa kwa wachezaji wake kujiuza.
Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji wa Kampuni hiyo, Abbas Tarimba alisema jana Dar es Salaam kuwa, ni jambo linalosikitisha timu za Tanzania kutolewa mapema katika michuano hiyo yenye dau kubwa zikionyesha wazi hazikuwa makini.
Timu za Tanzania zilizoshiriki michuano hiyo ni Yanga, Simba, Singida United na Jang’ombe Boys zilizoshindwa kutamba kwa timu za Kenya, Gor Mahia, AFC Leopards, Nakuru All Stars na Tusker. Simba ilitolewa hatua ya mtoano kwa penalti 5-4 dhidi ya Nakuru All Stars baada ya kutoka suluhu dakika 90.
Singida United ilitolewa na AFC Leopards kwa penalti 5-4 baada ya sare ya bao 1-1. Yanga iliwatoaTusker mchezo wa kwanza kwa penalti 4-2 baada ya kutoka suluhu 0-0 lakini ikatolewa nusu fainali na AFC Leopards kwa penalti 4-2 zilipotoka 0-0.
Akizungumza uwezekano wa kuzisaidia Simba na Yanga kucheza na Everton, Tarimba alisema ni mapema mno kulisemea hilo lakini wataangalia cha kufanya. “Hatukutarajia timu zetu zingetolewa mapema. Kwa kweli imetushangaza.
Tumeshindwa kucheza kwa kiwango cha juu jambo ambalo limetuhuzunisha. Inawezekana kabisa hazikufanya matayarisho,” alisema Tarimba. Alisema wachezaji wenyewe hawakuwa makini kwani ni kama walichezea bahati.
Alisema huenda hazikufanya matayarisho mazuri ingawa zilipewa taarifa mapema. Alisema hakubaliani na visingizio vya timu hizo kuwa wachezaji wao walikwenda kujiunga na timu ya Taifa, Taifa Stars kujiandaa na mechi ya AFCON dhidi ya Lesotho inayoanyika Chamazi, leo usiku.
Alisema hata Gor Mahia ina wachezaji wengi wanaocheza timu ya taifa Kenya na bado waliopo walicheza kwa kiwango cha juu na kufunga magoli katika mechi zao. Tarimba alisema ni Singida United tu iliyothubutu kufunga goli lakini si Simba, Yanga wala Jang’ombe iliyoweza kufanya hivyo zikionyesha udhaifu katika ufungaji.
Alisema lengo lao ni kusaidia soka la Tanzania na hasa wachezaji kufika mbali ndio maana walitoa fursa ya michuano hiyo ili wachezaji waitumie kuonyesha uwezo. Timu zilizotinga fainali ni Gor Mahia na Leopards zote za Kenya ambazo kesho zitacheza fainali na atakayeibuka bingwa atacheza na Everton Julai 13, mwaka huu.