Sura Mbili za Spika Ndugai Bungeni..!!!


Wakati wa Bunge la Bajeti la mwaka 2016/17, wabunge kutoka vyama vya upinzani walisusa vikao kila walipomuona Naibu Spika, Dk Tulia Ackson akiingia ukumbini.

Walisema Dk Tulia, ambaye alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu kabla ya kuteuliwa kuwa mbunge na baadaye kupitishwa na CCM kuwa mgombea nafasi ya Naibu Spika, alikuwa na uozefu mdogo na kutumia cheo chake kukandamiza upinzani.

Wakati huo, Spika wa Bunge, Job Ndugai alikuwa nje ya nchi kutibiwa na wengi walisikika wakisema kuwa kama mbunge huyo wa Kongwa angekuwepo, mambo yasingeweza kwenda kama yalivyokuwa yakiendeshwa na Dk Tulia.

Na baada ya kurudi nchini, Ndugai alihojiwa na kituo cha televisheni cha Azam na kusema kile wapinzani walichokitarajia.

Katika mahojiano hayo, Ndugai alisema kikao kilichokuwa kinafuata ambacho kilianza Septemba 6, 2016 angekitumia kufanya majadiliano kati ya Spika na Naibu Spika, wenyeviti wa Bunge pamoja na wabunge wa upinzani.

“Katika Bunge hili tuna malengo mengi kama changamoto ya kujenga Bunge moja na si vipande vipande. Kwa sasa ushirikiano umepungua bungeni, yaani kuna uvyama na migogoro imezidi, hii hali haiwapi raha Watanzania,” alisema Spika Ndugai akitoa matumaini kwa wapinzani.

Alifikia hata kuahidi kuwa ataazima kanuni za Bunge la Katiba lililompa mwenyekiti mamlaka ya kuunda kamati ya maridhiano ambayo ingefanya kazi ya kutafuta suluhisho kunapotokea matatizo.

“Kutoka nje ya bunge, si kosa ni haki ya kidemokrasia, lakini zipo njia mbalimbali za kufikisha ujumbe kwa mujibu wa kanuni zetu,” alibainisha.

“Mbunge wa upinzani anakatisha ruti (njia) ngumu kuliko mbunge wa CCM huko mtaani katika kugombea. Hukumbana na polisi na kupita sero, sasa anapofika pale bungeni subira inakuwa ndogo. Na akiguswa kidogo kumbukumbu yake inakuwa vile vile kuwa alah kumbe na huku ni walewale,” alisema Ndugai.

Takriban mwaka mmoja sasa, wapinzani wanaanza kuona sura tofauti ya Spika Ndugai. Sasa hawaoni uzoefu, kuwajali na wala kutenda haki sawa kwa wabunge wote.

Agizo lake la kutaka mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika atolewe kwa nguvu bungeni, kimeshawafanya wabunge wa upinzani kutathmini upya imani yao kwa Ndugai kulinganisha na ilivyokuwa miezi michache iliyopita na mwaka mmoja uliopita.

Miezi miwili iliyopita, Spika Ndugai alitumia maneno makali wakati akiagiza mbunge wa Kawe, Halima Mdee akamatwe kwa kosa la kumtukana, huku akiwaeleza wabunge kuwa chombo hicho kimeongeza uwezo wake wa kung’amua wakorofi ndani na nje ya ukumbi.

“Waheshimiwa wabunge, tumeimarisha sana masuala ya kujua mwenendo wa kila mmoja wetu ndani ya jengo hili na hata katika viwanja vyote vya Bunge, labda isipokuwa vyooni peke yake,” alisema Ndugai Aprili 6 mwaka huu.

“Lakini maeneo yaliyobaki mengine yote tuko imara na tuko vizuri sana, ningeliomba niwahakikishie waheshimiwa wabunge.

“Na yote hii ni kwa sababu ya usalama wenu na ulinzi wenu.

“Kwa hiyo ukiwa hapa ni vizuri ujue kuwa hauko jimboni wala mahali pengine. Bali mahali ambapo unapaswa kujiheshimu kibunge.”

Alikuwa akizungumzia tukio lililotokea Aprili 4 wakati wa kujadili uchaguzi wa wagombea wa nafasi tatu za upinzani katika Bunge la Afrika Mashariki, mjadala uliotawala na mhemko na hasira.

Katika mjadala huo, Mdee alisikika akisema neno “fala”, akilielekeza kwa Spika, hali iliyomfanya Ndugai kueleza jinsi walivyojizatiti kukabiliana na wabunge wanaozomea au kutoa lugha chafu.

“Niwaambieni nyinyi mnaomzomea Spika kwa mara nyingine na sitachoka kuwaambieni, tuna miezi hii, mitatu. Tutashughulika na kila mmoja ambaye anayedhani kwamba yeye kujifanya hapa ana (uwezo wa kufanya) vurugu,” alisema Ndugai.

Miezi miwili baadaye, Ndugai amekumbana tena na wabunge wanaozomea, lakini safari hii hawajakizomea kiti, bali Mnyika.

Akiomba mwongozo kwa Spika kuhusu madai ya mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde kuwa wapinzani wanatetea wezi katika suala la kuzuia mchanga wa madini kusafirishwa nje, Mnyika aligeuzia suala hilo kwa chama tawala akisema ndicho kilichoingia mikataba ya wizi na bado dhahabu inaendelea kusafirishwa nje.

Wakati Ndugai alipomtuliza kwa kumwambia hoja yake imesikika, sauti ilisikika kwenye kipaza sauti ikimuita Mnyika kuwa “mwizi” na mbunge huyo wa Kibamba akataka hatua zichukuliwe.

Lakini Spika hakutaka kuzungumzia sauti hiyo.

“Mheshimiwa Mnyika ulikuwa unaongea ukimuelekezea Mheshimiwa Lusinde. Mtu mwingine yeyote anayeongea kitu kingine hapa, mimi sina habari nacho. Mheshimiwa Lusinde endelea,” alisema Ndugai.

Lusinde alipotaka kuendelea, Mnyika naye alisimama na kuendelea kupaza sauti akitaka aliyesema neno hilo achukuliwe hatua, na ndipo Ndugai alipoamuru mbunge huyo wa Kibamba aondolewe kwa nguvu ukumbini.

Hadi jana hakukuwa na hatua zozote za kumtafuta mbunge aliyetoa neno hilo kwa kutumia mitambo ambayo Ndugai alisema ina uwezo wa kumtambua mbunge akiwa ndani au nje ya ukumbi wa Bunge.

Kitendo hicho kimewaudhi wapinzani na wanaona kuwa Spika ana sura mbili tofauti inapofikia masuala yanayowahusu wabunge wa CCM na wa upinzani.

“Ukiona wameungana na upinzani ujue wameguswa wao pia, lakini jambo likiwagusa upinzani pekee halina majibu mazuri zaidi ya dhihaka na majibu ya kuumiza upande mmoja,” alisema mbunge wa Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali.

“John Mnyika alipoitwa mwizi, (Spika) alikuwa hana masikio 100, lakini alipotukanwa yeye alikuwa na masikio 1,000 ya kusikia. Halikuwa kwenye hansard (kumbukumbu za Bunge) kama ambavyo wanapenda kujitetea, lakini kalisikia kwenye mitandao na akalitolea maamuzi.

“Lakini la Mnyika kuitwa mwizi hadharani tena kwa sauti ya wazi, halijatolewa maelezo zaidi ya aliyetukanwa kuonekana ana makosa na kutolewa nje. Kazi ya kututetea upinzani inabaki kwa wananchi.”

Hata hivyo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema kuangalia kwenye kamera kujua aliyetamka maneno “Mnyika mwizi” si busara, ingawa hakuunga mkono uamuzi wa Spika Ndugai.

Alisema angetumia ushawishi wake kulishauri Bunge kuchukua uamuzi tofauti kuliko chombo hicho kuwafungia wabunge wawili ambao wamechaguliwa na wananchi.

“Angeamua kwa busara hata kwa kusema aliyesema ameropoka na Mnyika atulie taratibu nyingine ziendelee badala ya kujibu kuwa hana masikio 100 ya kusikiliza huku na huku,” alisema Mbunda.

Alisema wakati mwingine nguvu hazihitajiki katika masuala ambayo yanaweza kumalizwa kwa kutumia busara, kama lilivyokuwa suala la Mnyika.

“(Mnyika) Ametukanwa na bado ametolewa nje na kadhia kadhaa zimetokea,” alisema Mbunda.

Kauli ya Mbunda inalingana na ya mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa aliyesema maamuzi hayakuwa ya haki kwa sababu Bunge lina uwezo wa kubaini aliyemtukana Mnyika.

Alisema hekima na busara vimekosekana katika Bunge badala yake utashi, uoga ndiyo vimetawala na kusababisha kinachosemwa kukinzana na kinachotendwa.

“Spika analinda heshima yake badala ya kulinda heshima na nidhamu ya mhimili wa Bunge kwa kuzingatia matakwa ya kidemokrasia,” alisema mchungaji huyo wa Kanisa la Vineyard.

“Vitisho wanavyopata kutoka kwa viongozi wao wa chama wanavileta hadi bungeni. Wanafanya kazi na kutoa maamuzi kwa uoga na kusahau haki.”

Msigwa alisema wakati mwingine kuwa wabunge ni kutumia vibaya fedha za wananchi kwa sababu kinachofanyika ni vurugu.

“Kwa mwenendo uliopo na unaoendelea wa kutisha wapinzani, kuwakatisha tamaa haina haja ya kuwa na Bunge,” alisema Msigwa.

Alieleza kuwa haina haja ya kuwa na kamera kama watu wanasema maneno ya kukera kwa wenzao na uwezekano wa kuwabaini upo, lakini haifanyiki.

“Kwa sababu aliyekerwa ni wa upinzani kamera hazina kazi na hazina maana kuwepo, lakini angekerwa wa chama tawala zingefanya kazi na kutegua kitendawili cha Mnyika,” alisema.

Ndugai na hasira

Pamoja na kuonyesha sura mbili, Ndugai anaonekana kuwa mtu mwenye hasira za karibu kwa jinsi alivyokuwa akizungumza katika matukio hayo mawili na mengine.

Wakati wa kura za maoni ndani ya CCM kuwania ubunge wa Kongwa, Ndugai aliingia kwenye mzozo na mgombea mwenzake kiasi cha kumpiga na fimbo aliyokuwa akitembelea wakati huo.

Alimshambulia kwa fimbo, Dk Joseph Elieza Chilongani katika mkutano uliofanyika Kitongoji cha Ugogoni.

Wakati mmoja wa wagombea akijinadi katika mkutano huo, alidai kuwa jimbo la Kongwa halijafaidika chochote kutoka kwa wachimbaji wa madini, jambo lililomuudhi Ndugai aliyekuwa amekaa kusubiri zamu yake na kumtaka mgombea huyo anyamaze kwa kuwa alikuwa anaongea upuuzi.

Wakati wawili hao wakiendelea kujibizana, Ndugai aligeuka na kugundua kuwa Dk Chilongani alikuwa akirekodi tukio hilo.

Ndugai aliamka huku akisema kuwa alikuwa akimtafuta siku nyingi Dk Chilongani na kwamba angemtambua kwa kurekodi tukio hilo.

Ndipo alipompiga kwa fimbo hiyo na baadaye kumshambulia, kabla ya kuamuliwa na baadaye Dk Chilongani kupelekwa hospitali kwa matibabu.

Wakati akitangaza uamuzi wa kumpeleka Mdee mbele ya Kamati ya Maadili ya Bunge, Ndugai alidokeza jinsi alivyojizuia hasira zake wakati akitukanwa.

“Watanzania wengi sana wameniandikia, wamesikitishwa sana, sana, sana na jambo hili. Na huu si utamaduni wa Watanzania, lakini kwa kuwa wenzetu wamefika hapo,” alisema.

“Na hii si mara ya kwanza kwa Halima na hata juzi nilivumilia sana. Yaani nilivuta, nikamuomba Mungu anisaidie. Nikanyamaza kimya.”

Kutenda haki

Spika Ndugai pia ameonyesha kutenda haki katika baadhi ya matukio.

Aliwahi kumtimua ukumbini mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk Faustine Ndungulile kwa kosa la kumuita Mdee kuwa ni kituko.

Pia mapema mwaka huu alikemea vitendo vya kukamatwa ovyo kwa wabunge akisema jambo hilo ni kinyume cha sheria na utaratibu. Akihitimisha Mkutano wa Sita wa Bunge, Ndugai alisema kama kuna kiongozi yeyote wa Serikali anamuhitaji mbunge, anapaswa kutoa taarifa kwake kwanza badala ya kwenda moja kwa moja kumkamata.

Ilikuwa ni baada ya wabunge kama Tundu Lissu na Godbless Lema kukamatwa na kusafirishwa kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka, huku Zitto Kabwe akiamua kugomea ndani ya viwanja vya Bunge ili asikamatwe.

Habari ya ziada na Kalunde Jamal (kjamal@mwananchi.co.tz)     
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad