SIMBA imeamua kufanya kufuru katika usajili wake kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo inasemekana wametumia dau la Dola 50,000 za Marekani (Sh mil 110) kwa ajili ya kumng’oa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Haruna Niyonzima.
Niyonzima ambaye amemaliza mkataba wake na Yanga, yupo nchini kwao Rwanda alipokwenda kuungana na timu yake ya taifa ‘Amavubi’ kwa ajili ya mechi ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon).
Yanga imeshindwa kuwaongezea mikataba mipya baadhi ya wachezaji wake wa kimataifa kutokana na kile kinachodaiwa ni ukata ulioikumba klabu hiyo kwa sasa.
Kufuatia jambo hilo, uongozi wa klabu ya Simba ambao kwa muda mrefu walikuwa wakihitaji huduma na Mnyarwanda huyo, umefunga safari hadi nchini kwao kwa ajili ya kumalizana na mchezaji huyo.
Akizungumza kwa njia ya simu kutokea Rwanda, mmoja wa wanafamilia wa mchezaji huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema tayari viongozi wa Simba wamemalizana na mchezaji huyo kwa dau la dola 50,000 za Marekani.
Alisema: “Ni kweli Niyonzima amemalizana na Simba na wamemfuata huku na hivyo kila kitu kimekwenda sawa.”
Kwa upande wake, Niyonzima licha ya kuthibitisha viongozi wa Simba kumfuata kwao nchini Rwanda, lakini alisema bado hajaingia mkataba rasmi na timu hiyo.
“Ni kweli viongozi wa Simba wamenifuata Rwanda, nimerudi juzi kutoka kuitumikia timu yangu ya Taifa, sijasaini mkataba nayo lakini tupo kwenye mazungumzo,” alisema Niyonzima ambaye ni nahodha wa Amavubi.
Hata hivyo, hivi karibuni mchezaji huyo alihojiwa na gazeti la New Times Sports la nchini kwao na kuweka wazi mipango yake akisema, ameshawaaga mashabiki wa Yanga na kwamba muda wake wa kuondoka ndani ya timu hiyo umefika.