Timu Yakamilisha Uchunguzi Sakata la Pacha Temeke


Timu iliyoundwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kuchunguza tuhuma za wizi wa mtoto pacha katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke, imekamilisha kazi yake.

Habari zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa timu hiyo, Profesa Charles Majinge zilieleza uchunguzi ulikamilika mwishoni mwa juma lililopita na wakati wowote ripoti itakabidhiwa kwa waziri.

Waziri Mwalimu aliunda timu hiyo Mei 29, mwaka huu baada ya familia inayodai kuibiwa mtoto kutoridhika na ripoti ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Grace Magembe iliyoeleza mlalamikaji hakuwa na pacha, bali watumishi wa hospitali hawakutimiza wajibu wao, hivyo kumfanya aamini alikuwa na pacha.

Waziri aliunda na kutangaza timu hiyo baada ya kukutana na familia inayodai kuibiwa mtoto ya Asma Juma na Abubakar Pazi.

Profesa Majinge aliliambia gazeti hili kuwa wameshakamilisha ripoti na wanasubiri maelekezo ya waziri ili kumkabidhi.

“Tumeshakamilisha ripoti yetu na kama waziri angekuwapo tungemkabidhi hata Ijumaa, kwa sasa nataka nifanye mawasiliano na katibu wake ili atueleze lini tumkabidhi,” alisema Profesa Majinge.

Timu hiyo ilitakiwa kufanya kazi kwa muda wa siku 14 kuanzia Mei 31 na kukabidhi ripoti Juni 14.

Timu hiyo ilikutana na walalamikaji Muhimbili Juni 3 na baadaye kuendelea na uchunguzi kwa kuwahoji walalamikiwa ambao ni madaktari waliohusika kumpasua mama huyo alipojifungua, wahudumu wengine wa afya katika Hospitali ya Temeke na zahanati ya Mbande alikokuwa akipata huduma za kliniki.

Pia ilifanya mahojiano na mtaalamu wa vipimo vya ultrasound katika zahanati ya Huruma iliyoko Mbande na kutembelea na kukagua zahanati na mashine hiyo.

 
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad