Ubuyu huu siyo wa nchi hii! Mkongwe wa filamu na tamthiliya za Kibongo, Tuesday Kihangala ‘Chuz’, yupo katika wakati mgumu baada ya kutuhumiwa kisha kudaiwa kukamatwa na polisi kwa tuhuma nzito ya rushwa ya ngono, Wikienda limesheheni.
Wikiendi iliyopita gazeti hili lilipokea ‘mapovu’ ya vyanzo vyake kutoka kona mbalimbali ndani na nje ya Bongo, yakimtuhumu staa huyo kuwatumia kingono wasanii wa kike, wenye tamaa ya kuchomoka kisanaa.
Chuzi anayetamba na Tamthiliya ya Closed Chapter inayoruka kupitia TBC1, alidaiwa kuwafanyia wasanii wa kike 33, wakiwemo mapacha, vitendo hivyo vya kingono huko Lushoto mkoani Tanga alikoweka kambi kwa ajili ya maandalizi ya tamthiliya yake mpya.
Ilidaiwa kwamba, Chuz amekuwa akiwalazimisha kuwatumia kujistarehesha na wale wanaokataa huwafukuza kambini.
Wakati tuhuma hizo zikikolea mithili ya moto wa kifuu, Wikienda lilipokea sauti ya mwanaume aliyejitambulisha kama mmoja wa wasanii waliokuwa kambini ikidai kuwa, alishuhudia wasanii wa kike ambao ni chipukizi kutoka mkoani Arusha wakidhalilishwa kingono na Chuz.
“Kiukweli kuna wasanii wa kike wanateseka sana kambini anakoshuti Chuz. Vitu vinavyoendelea ni udhalilishaji hasa kwa mabinti wadogo ambao wametoka Arusha.
“Tulimwacha dada yetu mmoja kambini kule Lushoto, sisi tukarudi Arusha. Sasa hivi yupo njiani anarudi Arusha.
“Ukweli ni kwamba, Chuz hawezi kumpa binti scene (kipande cha kuigiza) bila kuwataka kimapenzi, yaani mtu alipokuwa akiingia kwa Chuz anakaa saa mbili anafanyishwa hayo mambo yake.
“Tunaomba viongozi wakawasaidie wasichana waliobaki kule Lushoto, kiukweli imeniuma sana na
ndiyo maana naongea haya. Chuz anawadhalilisha wasanii wa kike, wakimkataa anawaundia zengwe, anawafukuza.
“Amekuwa akisema kuwa anafanya hivyo kwa sababu alishaumizwa sana na wasanii wa kike hivyo analipiza, yaani mwanamke akimkataa anamfukuza, scene zinaanzwa upya, tunamuomba Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Simon Mwakifwamba aliangalie hili,” ilisema sauti hiyo ya kijana aliyejitambulisha kwa jina la Edward ambaye ni mkazi wa Arusha huku akisema ana mengi mno ya kuelezea aliyoyaona kambini kwa Chuz.
WASANII WAJA JUU
Baada ya sauti hiyo kusambaa, wasanii mbalimbali wa tasnia hiyo Bongo walikerwa na kitendo hicho na kusababisha kuunda Kundi la WhatsApp huku wakimjadili Chuz na yeye akiulizwa kulikoni kufanya hivyo, lakini muda mwingi alikuwa akisema yuko bize na kazi.
AUNDIWA TUME
Baadhi ya wasanii kupitia kwa Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji Tanzania, Elia Mjata, wameunda tume ya kumchunguza Chuz kama ile ya kuchunguza mchanga wa dhahabu ‘makinikia’.
Tume hiyo inaongozwa na msanii wa filamu za Kibongo, Michael Sangu ‘Mike’ na wajumbe wengine huku majina mengine kutoka taasisi za kiserikali yakisubiriwa ili kazi ya uchunguzi ianze mara moja.
Akizungumzia skendo hiyo, Mike alisema kuwa, kwa sasa wanajiandaa huku wakiwasubiri hao wajumbe wa taasisi za serikali ambapo uchunguzi wa kina utafanyika kuanzia Lushoto ilipo kambi ya Chuz kwani tuhuma hizo ni nzito.
CHUZ AKAMATWA, AACHIWA
Habari nyingine kutoka Lushoto zilidai kwamba, baada ya kuenea kwa ishu hiyo, Chuz alikamatwa na polisi na kuhojiwa hukohuko Lushoto na kuachiwa, haikujulikana alihojiwa nini na aliachiwa kwa maelezo gani.
“Polisi walifika kambini wakamkamata na kwenda naye kituoni, lakini baada ya muda alirejea mzigoni. Hakuna anayejua kilichoendelea huko,” kilisema chanzo kingine.
CHUZ ANASEMAJE?
Ili kupata mzani wa ubuyu huo, Wikienda lilimtafuta Chuz na kumsomea tuhuma hizo ambapo mambo yalikuwa hivi;
Wikienda: Kuna habari kwamba umewafanyia udhalilishaji wa kingono wasanii wa kike na wale
wanaokataa unawafukuza kambini, hili likoje?
Chuz: Siyo kweli, hakuna hata mmoja aliyefukuzwa.
Wikienda: Kuhusu suala hili la kuwatumia kimapenzi vipi?
Chuz: Huyo dogo (mwanaume) ambaye amejirekodi hiyo sauti, aliondoka kambini, alipotaka kurudi hatukuwa tayari kwa kuwa muda wa ruhusa yake uliisha, ndiyo maana anafanya hivyo.
Wikienda: Na hao wasichana uliowatumia kingono wakiwemo mapacha na wasichana wengine wawili vipi?
Chuz: Kuhusu uhusiano, sidhani kama ni habari mpya, imeshaandikwa sana.
Wikienda: Kuna madai kuwa unawatumia kinyume na maumbile, je, hili likoje?
Chuz: Hilo hata Mungu atanihukumu kama nitafanya huo uchafu.
Wikienda: Unafikiri chanzo cha tuhuma hizi nzito ni nini?
Chuz: Chanzo ni huyo msanii wa Arusha baada ya kumkatalia kurudi kambini.
Wikienda: Kuna madai kuwa ulikamatwa na polisi, je, ni kweli?
Chuz: Ni kweli, walinifuata polisi, nikaenda kituoni kwa mahojiano.
Wikienda: Polisi walikuhoji kuhusu nini?
Chuz: Ni mambo ya uchunguzi nisingependa kuyazungumzia.
NENO LA MHARIRI
Ubuyu ndiyo huo na mambo yameanza kupamba moto hivyo ili kupata ukweli, tuvute subira, uchunguzi ufanyike na majibu utayapata kupitia Magazeti ya Global Publishers, usicheze mbali.
Ubuyu: Gladness Mallya | Ijumaa Wikienda