Wabunge wa CCM na Upinzani Watofautiana Kuhusu Bajeti ya Serikali...!!!


Wabunge wa CCM wameipongeza bajeti ya mwaka wa fedha 2017/18 wakisema inalenga kuondoa kero za wananchi wa hali ya chini huku wenzao wa upinzani wakisema ni bajeti ya maumivu kwa watu wa hali ya chini baada ya mafuta kuongezeka.

Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti mara baada ya bajeti hiyo kusomwa bungeni jana, wabunge wa CCM walisema bajeti hiyo imemaliza kila kitu.

Mbunge wa Sumbawanga Mjini (CCM), Aeshi Hilaly alisema bajeti hiyo imekidhi matakwa ya wabunge ingawa bado hawajafahamu wananchi wataipokea vipi.

“Kimsingi yale tuliyokuwa tunayapinga mwaka jana, mwaka huu wameyaondoa. Nataka nimpongeze waziri ameleta bajeti nzuri sana tumeipokea kwa mikono miwili. Kazi iliyobaki ni kwenda kuipitia ili maeneo ya kurekebisha tufanye hivyo.

Mbunge wa Lupa (CCM), Victor Mwambalaswa alisema katika kipindi cha miaka 15 aliyokuwa ndani ya Bunge haijawahi kutokea bajeti nzuri iliyowalenga wananchi wa chini kama ya mwaka huu.

“Kwa mfano maeneo ya kodi katika mazao ya wakulima, pembejeo, mbolea na kodi za magari za kila mwaka. Ingekuwa ni uwezo wangu mimi hatuhitaji hata kuijadili, sema Katiba inasema tujadili,” alisema.

Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea alisema kuwa ni jambo zuri kwa Serikali kuondoa kodi za magari za kila mwaka lakini kwa kuifidia katika mafuta kunalenga kumuongezea mzigo mwananchi wa hali ya chini.

“Eneo jingine ni kutegemea misaada kutoka nje na bahati mbaya wafadhili huwa hawatimizi masharti. Kuondoa kodi ya mabango kwenye halmashauri na kuipa TRA (Mamlaka ya Kodi Tanzania) jukumu la kukusanya, inaonyesha kuwa kuna njama katika halmashauri zinazoongozwa na wapinzani,” alisema na kufafanua:

“Halmashauri zenye mabango nyingi zipo mjini na zinaongozwa na upinzani. Hizi ndizo kodi kubwa ambazo halmashauri ilikuwa inategemea.”

Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia alisema bajeti hiyo ni changa la macho kwa sababu asilimia 37 ya fedha inategemea mikopo yenye masharti nafuu na misaada kutoka nje ya nchi.

“Pia Deni la Taifa limekua kutoka Sh39 trilioni hadi Sh50 trilioni, kwa maana hiyo kila Mtanzania anadaiwa zaidi ya Sh1 milioni,” alisema Mbatia.

“Ni maumivu kwa Watanzania, ni wangapi ambao wana magari lakini kwa kupeleka kodi ya magari katika mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa inamaanisha gharama za kusaga, usafiri na usafirishaji zitaongezeka,” alisema

Mbunge wa Mtwara Mjini (CUF), Maftaha Nachuma alisema ni bajeti ambayo imeakisi matakwa ya wananchi kwa kuondoa ushuru ambao ni kero kwenye maeneo mbalimbali.

“Kuondoa ushuru katika bidhaa zinazosafirishwa nje ya nchi ndiyo kilio chetu, sasa kitafanya watu ambao walikimbia kutumia bandari zetu kurejea na hivyo kukuza uchumi wa nchi,” alisema.

Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiku alisema kuondoa kodi ya mabango katika halmashauri kutashusha makusanyo ya halmashauri.

“Hizi halmashauri zilikuwa tayari zimepanga bajeti zao. Je, kulikuwa na mawasiliano kati ya halmashauri na Serikali Kuu kuhusu maeneo haya waliyoyaondoa kodi?” alihoji.     

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Kupinga hiyo ndio shughuli ya upinzani.
    Kama nimeielewa vizuri hiyo kodi ya mabando ilofutwa, ni yale mabango yanayoelekeza kwenye huduma za kijamii kama hospital, shule n.k.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad