Dodoma. Wabunge wa chama tawala wameunga mkono ripoti ya Taasisi ya Twaweza inayoeleza kushuka kwa ushawishi wa Rais John Magufuli.
Ripoti hiyo iliyotolewa jana na kubainisha kwamba umaarufu wa Rais huyo wa awamu ya tano umeshuka na kwamba anakubalika miongoni mwa maskini, wasio na elimu kubwa pamoja na waishio vijijini.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Lucy Mayenga amesema kilichoelezwa na Twaweza ni sahihi kwa sababu Rais amejielekeza kwa makundi hayo ambayo hayana mtetezi.
"Hao ndiyo watu wengi zaidi. Kiuchumi inakubalika," amesema Lucy.
Wakati Lucy akiendelea kutoa hoja zake, Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega alitoa taarifa iliyopokelewa na mtoa hoja.
Uledi amesema: "Kwa muda wa utafiti, Rais alikuwa anapambana na vyeti feki, dawa za kulevya na mafisadi. Hao wote hawawezi kumpenda zaidi ya maskini ambao hawaguswi na mambo hayo."
Lucy ametoa maoni hayo wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Serikali unaoendelea bungeni.