Wabunge Walilia Bei ya Bia na Soda Zisipande Bei Kwenye Bajeti Kuu ya Serikali Itakayosomwa Kesho..!!!


WAKATI Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/18 ikitarajiwa kuwasilishwa bungeni kesho, baadhi ya wabunge wametoa maoni yao wakisisitiza haja ya sekta ya maji na sekta ndogo ya umeme kupewa fedha nyingi.

Aidha, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) amependekeza kupunguzwa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), na kuondolewa kwa kodi hiyo katika malighafi za kilimo zinazozalishwa nchini, na kusiwepo upandishaji wa ushuru wa vinywaji baridi na bia.

Wabunge wametoa maoni hayo wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ikiwa katika mashauriano na serikali kwa siku ya tatu kuhusu hoja zilizojitokeza wakati wa kujadili bajeti za kisekta bungeni.

Kamati hiyo ya Bajeti chini ya Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia (CCM), imekuwa katika majadiliano hayo na serikali ili kuboresha maeneo ambayo wabunge walitaka yafanyiwe kazi kabla ya Bajeti ya Serikali kusomwa kesho.

Kesho asubuhi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango atawasilisha bungeni Taarifa ya Hali ya Uchumi nchini kabla ya jioni kuwasilisha Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/18.

Akizungumza na gazeti hili, Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi (CCM) alisema suala la maji ni muhimu, hivyo serikali haina budi kuongeza fedha badala ya kupunguza, kama ilivyofanya bajeti ya wizara hiyo kutoka zaidi ya Sh bilioni 900 hadi zaidi ya Sh bilioni 600.

Aidha, Chumi alilitaja eneo jingine ambalo serikali inatakiwa kulitazama ni kuchangia katika ujenzi wa maboma ya zahanati, vituo vya afya na madarasa. “Serikali ilihamasisha wananchi wajenge maboma hayo na wao watamalizia, kazi hiyo imefanyika lakini serikali haijaweka fedha katika maeneo mengi, hii inaweza kukatisha tamaa wananchi siku nyingine watakapoombwa kuchangia,” alieleza Chumi.

Lakini, pia alitaka serikali itenge fedha kwa ajili ya Mfuko wa Mazingira hasa baada ya hali ya sasa ya mabadiliko ya tabianchi, ambayo yameathiri maeneo mengi nchini. “Fedha hizi zitasaidia katika kutoa ruzuku kwa maeneo yenye kufanya vizuri katika uhifdhi wa mazingira na hivyo kuchochea watu wengine kupanda miti kwa wingi na hivyo kurejesha hali ya kijani,” aliongeza Chumi.

Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Mollel (CCM), alitaka kuwapo kwa msamaha wa kodi kwa watu wenye ulemavu hasa katika vifaa vyao. Mollel alisema mbali ya msamaha huo, pia serikali kuimarisha Mfuko wa Watu wenye Ulemavu hasa baada ya kuunda Baraza la Watu wenye Ulemavu nchini.

Aidha, Mollel alipendekeza kwa serikali kutenga asilimia mbili kutoka katika asilimia 10 iliyotengwa katika halmashauri kwa ajili ya mifuko ya vijana na wanawake, iende kusaidia watu wenye ulemavu.

Mbali ya hayo, alitaka wizara nyeti ikiwamo ya Nishati na Madini kuongezewa fedha hasa wakati huu, ambao amesema Rais John Magufuli anapambana kuhakikisha rasilimali za Taifa yakiwamo madini yanawanufaisha Watanzania badala ya wachache kunufaika.

Kwa upande wake, Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM), alisema maji na nishati ya umeme ni muhimu na akapendekeza kuundwa kwa Mfuko wa Maji Vijijini. Ndassa alisema kama ilivyo kwa umeme ambako kuna Wakala wa Umeme Vijijini (REA), ni muhimu kuwa na Mfuko wa Maji Vijijini ambao utawezeshwa na tozo ya mafuta kupandishwa kutoka Sh 50 hadi 100.

“Fedha hizi zitakazopatikana ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 360 ziwekwe zisiguswe kwa kazi nyingine, zitumike kwa ajili ya Mfuko wa Maji Vijijini, maji ni muhimu pengine kuliko umeme,” alieleza Ndassa.

Alishauri serikali kuendelea kuweka mazingira mazuri ya ukusanyaji wa kodi na kuwa na vyanzo vyake vya kuaminika vya mapato ili Taifa lijitegemee lenyewe. Mbunge wa Bukombe, Dotto Biteko (CCM) pia alikazia suala la maji, umeme, kilimo na ardhi, akisisitiza fedha nyingi zielekezwe katika miradi ya maji nchini kwani maji ni muhimu kwa matumizi ya binadamu na kilimo.

Biteko alisema kuwapo kwa maji ya kutosha yatawezesha kufanyika kwa kilimo cha umwagiliaji, hivyo kuzalisha malighafi nyingi kwa ajili ya Tanzania ya viwanda. Katika kilimo alipongeza serikali kwa kuondoa tozo zilizokuwa na kero kwa wananchi, kama ilivyofanya katika ardhi, hivyo kuwataka wananchi watumie fursa hiyo kujiongezea uzalishaji wao na kujiletea maendeleo.

Kuhusu umeme, alisema serikali imeahidi kuvipatia umeme vijiji vyote nchini mwaka huu, hivyo akataka Bajeti ya Serikali itenge fedha kuharakisha azma hiyo. Hoja ya umeme na maji pia ilitolewa na Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM), akisema maji ni kila kitu, ni vyema kuongeza fedha katika sekta hiyo na umeme.

Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Lupembe (CCM) pia alizungumzia suala la maji, akisema maenep mengi nchi yana tatizo kubwa la maji, hivyo akashauri fedha za bajeti ziongezwe ili kuhakikisha miradi mingi ya maji inaanzishwa au inakamilishwa kwa haraka.

Nkamia pia alitoa pendekezo la kuanzishwa kwa dirisha maalumu la serikali katika Bandari ya Dar es Salaam ili kurahisisha utoaji wa vifaa vya serikali bandarini. Kwa upande wake, Bashe alipendekeza katika bajeti ya kesho serikali ipunguze VAT hadi kufikia asilimia 16 kutoka 18 ya sasa na iondoe kodi hiyo katika bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.

Bashe pia alitaka VAT iondolewe katika malighafi za mazao yanayozalishwa nchini, na kusiwapo na ushuru wa bidhaa katika pembejeo za kilimo. “Kwa kufanya hivyo, uzalishaji utaongezeka, serikali itapata kodi nyingi (kodi ya makampuni, VAT na kodi ya ushuru wa forodha).

Hii pia itaongeza ajira na hivyo kusaidia kupata kodi ya PAYE,” alieleza Bashe. Akijibu swali bungeni juzi, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji alieleza kuwa serikali itawasilishwa katika bajeti yake mapendekezo ya kufuta misamaha ya kodi isiyo na tija.

Dk Kijaji alisema mpango wa serikali ni kuhakikisha misamaha ya kodi inashuka mwaka hadi mwaka na katika mwaka ujao wa fedha, serikali italeta mapendekezo ya marekebisho ndani ya bajeti itakayosomwa kesho.

Machi 29, mwaka huu, Dk Mpango alisoma mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na kiwango cha ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa 2017/18. Kwa mujibu wa Dk Mpango, serikali katika bajeti hiyo inatarajia kuwa na ukomo wa Sh trilioni 31.6.

Katika fedha hizo, za maendeleo zimeongezeka kutoka Sh trilioni 11.8 katika mwaka 2016/17 hadi Sh trilioni 11.9 katika mwaka wa bajeti 2017/18. Ongezeko hilo ni kiasi sawa na asilimia 38 katika bajeti hiyo tarajiwa.

Credit -Habari Leo
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. tulishaacha kunywa bia na soda....waangalie bei za mafuta ya diseli na petrol kwanza nyambaf

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad