MHADHIRI Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Banna, amesema adhabu iliyotolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wabunge wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Halima Mdee na Ester Bulaya ya kufungiwa shughuli za Bunge kwa takriban mwaka mmoja ni sahihi.
Wabunge hao walipewa adhabu hiyo juzi kwa kosa la utovu wa nidhamu katika kikao cha Bunge na kukidharau Kiti cha Spika, Ijumaa iliyopita. Wabunge hao walionesha utovu huo wa nidhamu bungeni, wakipinga Mbunge wa Kibamba, John Mnyika kutolewa nje ya Bunge kwa agizo la Spika wa Bunge Job Ndugai.
Kutokana na Mnyika kukaidi amri ya Spika ya kumtaka akae huku Mnyika akitaka ombi lake la utaratibu bila kujali maelekezo ya Spika, Ndugai aliagiza askari kumtoa nje ya Bunge na kutohudhuria vikao vya Bunge kwa wiki moja.
Wakati askari wakimtoa Mnyika ukumbini, Halima ambaye ni mbunge wa Kawe na Bulaya wa Jimbo la Bunda Mjini, waliinuka katika viti vyao na kuelekea upande wa askari waliokuwa wakimtoa nje Mnyika huku Bulaya akihamasisha wabunge wengine wa upinzani kuondoka na kususa Bunge.
Kutokana na hali hiyo, Ndugai aliiagiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kujadili adhabu mwafaka na ndipo baada ya mjadala, Bunge likaridhia wabunge hao kutoshiriki shughuli za Bunge vikiwamo vikao vya Bunge na safari na vikao vya Kamati za Kudumu hadi mwezi Aprili mwakani katika Bunge la Bajeti mwaka 2018/ 2019.
Akizungumza na gazeti hili, Dk Banna alisema wabunge hao walidhalilisha Bunge, wapiga kura na wananchi katika majimbo yao. Alisema wabunge wanapaswa kuheshimu kanuni za Bunge na kuzifuata ili kufanya uwakilishi mzuri kwa wananchi.
“Kuna gharama ya kuwa Mheshimiwa na hiyo ni kuwa na hekima kwa kuwa chochote kinyume na hapo ni kosa tena kubwa na wabunge hao wamevuna kile walichokipanda,” alisema.
Mbunge wa Kaliua wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya alisema kuwa adhabu hiyo ni mwafaka kwa wabunge hao kutokana na kuwa walikwishaonywa. Alisema, Bunge linatakiwa kuheshimiwa na wabunge hao wamekuwa watata mara kwa mara katika kufuata kanuni zilizowekwa.
Alisema, wabunge wanatakiwa kuwa na nidhamu, uvumilivu na hekima ya hali ya juu kipindi chote wakati Bunge likiwa linaendelea. Alisema kwa upande wa Mdee, ndani ya kipindi kifupi amefanya makosa kadhaa ya utovu wa nidhamu.
Alisema, mbunge huyo aliitwa kwenye kikao cha Kamati ya Nidhamu mwezi Aprili baada ya kudaiwa kumtukana Spika Ndugai na alipewa karipio kali la kumtaka asirudie kosa. Alisema wakati wakiwa kwenye kikao hicho, aliambiwa wazi kuwa iwapo atarudia tena kosa, atapewa adhabu kali zaidi na kwa sasa anatumikia kile alichoonywa.